Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amewataka watendaji waliopewa dhamana kwa niaba ya Watanzania kubadilika la sivyo watabadilishwa kama utendaji wao hautaakisi dhamira ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo kwenye kikao chake cha kwanza na menejimenti ya Wizara hiyo tangu alipoteuliwa na Rais Samia kushika wadhifa huo.
“Mara zote ninapopata uteuzi wa Rais napongezwa lakini ni Wizara hii ambapo nimekuwa nikipongezwa na pia kupewa pole; pole hizi zinamaana kwamba taswira ya wizara hii muhimu kiuchumi kwa nchi sio nzuri. Kwanini kuwe na makandokando?
“Sasa kama alivyosema Mhe Waziri wetu, Mohamed Mchengerwa siku anakabidhiwa ofisi hapa kwa sasa kuna kazi kubwa ya kusafisha taswira ya Wizara hii kwa kuchapa kazi kiuadilifu na watu waone matokeo. Waziri alisema nami nasisitiza leo hakutakuwa na namna ya mtu kukwamisha azma hii ya kuisafisha wizara hii ya kimkakati,” alisema Dkt. Abbasi.
Katika kuhakikisha watendaji wa Wizara hiyo wanabadilika kutoka utendaji wenye mauzauza hadi kuwa na utendaji wa kuwajibika kwa maslahi ya nchi.
Dkt. Abbasi alitumia zaidi ya saa nzima kuwapa Siri Nane za kuleta mabadiliko (8 Secrets of Transfotmation), ambazo watendaji hao watapaswa kubadilika, kuishi nazo na kupimwa nazo, siri ambazo watendaji hao walionesha kuridhika nazo huku wakiahidi kuzitumia katika “maisha yao mapya.”
Sekta ya Maliasili na Utalii inachangia asilimia 25 ya Fedha za Kigeni kwa Serikali na takribani asilimia 21 ya Pato la Taifa.