Mhe. Mchengerwa- Serikali kuwashirikisha wadau kwenye mnyororo wa thamani wa utalii.


Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imedhamiria kufanya kazi kwa pamoja na wadau mbalimbali wa utalii nchini kwa ajili ya kuimarisha mahusiano ya serikali na wadau (Public Private Partnership) ili kufikia kwa haraka   lengo la  kuwapata  watalii  milioni tano hatimaye  kuchangia  kwenye uchumi wa nchi.

Akizungumza kwenye Tamasha la Kwanza la Biashara la Wadau wa Utalii leo, Februari 23, 2023 lililopewa  jina la “The Z sumit” ambapo Rais wa Zanzibar, Mhe. Hussein Mwinyi amekuwa Mgeni Rasmi, Mhe. Mchengerwa amesisitiza kuwa  dhamira ya serikali kwa sasa ni kuwashirikisha wadau  wote  kwenye mnyororo wa thamani wa utalii ili kutoa huduma  ya kiwango cha kimataifa kitakachowavutia watalii kuja kujionea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini.

Aidha, amemhakikishia Mhe. Rais Mwinyi kufanya kazi kwa karibu na Waziri anayesimamia sekta ya Utalii kwa upande wa Zanzibar katika kupanga mikakati ya pamoja ya kutangaza vivutio vya utalii ikiwa ni pamoja na kuwaalika watoa huduma za utalii wakubwa  duniani  ili  kutengeneza mnyororo mzuri wa thamani wa utalii. 



Amesema kwa ukubwa wa Tanzania na kwa uwingi wa vivutio vilivyopo bado kuna kazi kubwa inayotakiwa kufanywa  kwa  pamoja  baina  ya Serikali na wadau ili sekta ya utalii iweze kuchangia kiasi kikubwa kwenye pato la taifa.

“Kwa ukubwa wa nchi yetu na historia ya nchi yetu hatupaswi kuwa nyuma nina imani tuna kazi kubwa ya kufanya kuitangaza nchi yetu, kwani idadi ya watalii wanaoingia  nchini bado  kwetu ni aibu kubwa  katika sekta zetu kwa hiyo tuna kazi kubwa sana ya kufanya kuwakaribisha wageni  kutoka nchi mbalimbali duniani .” amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Aidha, amefafanua kwamba wakati umefika wa kuainisha vivutio vingine vya  utalii kama utalii wa michezo na utamaduni pia kubuni mikakati  kabambe ya  kidigitali  ya kuutangaza  utalii  kimataifa.

Akitolea mfano amesema nchi ya China hutoa watalii takribani milioni mia moja na hamsini  lakini wanaofika Tanzania ni elfu arobaini na tano tu na kusisitiza kuwa  vilevile  kunahitajika kazi kubwa ya kuboresha  miundombinu ya utalii.

Tamasha hili la kwanza la wadau wa utalii limeratibiwa  kwa pamoja na kampuni ya Kilifair  kutoka Tanzania Bara na ZATI kutoka Zanzibar kwa lengo  la kuandaa jukwaa la kuwakusanya wadau mbalimbali wa utalii kuja kubadilishana uzoefu na kufanya biashara, ambapo litakuwa likifanyika kila mwaka.

Post a Comment

Previous Post Next Post