PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
***************
SERIKALI Imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) katika Sera pamoja na kuingia mikataba na taasisi za kifedha ili kuwapa nguvu kutokana na kazi bora wanayoifanya ya kuwasaidia watanzania katika kubuni, kusimamia na kujenga majengo mbalimbali ya makazi na biashara.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi ‘ Magomeni Kota Phase 2 A’ uliokamilika kwa asilimia 96 Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi. Godfrey Kasekenya amesema mradi huo wa kisasa utaanza matumizi yake kufikia mwezi ujao.
“Mradi huo wa kisasa una ghorofa nane utabeba Kaya kumi na sita kwa kaya mbili kila ghorofa ambazo zina huduma zote muhimu umebuniwa na kutekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) ambayo Serikali imeiamini zaidi katika kujenga majengo kwa ajili ya makazi na biashara”. Amesema
Kuhusiana na uhitaji wa nyumba hizo za makazi Kasekenya amesema, hadi sasa watumishi wengi wamejitokeza kuomba kupanga nyumba hizo hali inayoashiria uhitaji mkubwa wa majengo ya makazi kwa watumishi na wasio watumishi na kuiagiza TBA kushirikiana na taasisi binafsi katika kupunguza changamoto hiyo na Serikali itashirikiana nao hususani katika Sera na kuingia mikataba na taasisi za kifedha.
“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa tayari na mstari wa mbele katika kuanzisha na kuendeleza miradi ambayo anaamini itawasaidia wananchi wakiwemo watumishi… Serikali imejipanga katika hili na Wizara hatujakwama fedha zinakuja na miradi inatekelezwa.” Amesema Kasekenya.
Aidha, ameeleza kuwa mradi huo hadi kukamilika kwake utagharimu shilingi Bilioni 5.6 na majengo mengine matano yanajengwa katika eneo hilo kwa ajili ya watumishi ambapo wa ujumla Kaya 80 zitaishi katika eneo hilo huku mradi unaotekelezwa katika eneo la Temeke Mwisho ukitegemewa kubeba Kaya 148.
Pia ameitaka TBA kupitia watendaji wake kuwa waadilifu kwa kujenga majengo yenye thamani ya fedha inayotolewa na Serikali na kutotumia fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo vinginevyo.
“Ikiwezekana endeleeni kutumia vifaa vya ujenzi vya hapa Tanzania, wataalam tuwe wabunifu wa vifaa vya ujenzi bila kutegemea kuagiza kutoka nje… Na watakaopata nafasi ya kuishi katika nyumba hizi watunze mazingira haya ili kupunguza gharama ya kuyatengeneza mara kwa mara.” Amesema.
Vilevile amesema mradi huo unategemewa sana na wananchi wakiwemo watumishi ambao wanahitaji makazi bora na salama ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na TBA wamekuwa wakipunguza changamoto hiyo ya makazi kwa kutekeleza miradi hiyo kwa ubunufu na usasa zaidi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) Arch. Daud Kondoro amesema uhitaji wa nyumba za makazi kwa wananchi wakiwemo watumishi bado ni changamoto na Wakala hiyo inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa nyumba za makazi na biashara kupitia fedha za ruzuku.
Arch. Kondoro amesema, TBA inazingatia matumizi fedha kwa kuhakikisha fedha zinazotolewa zinatumika ipasavyo kwa kuzingatia thamani na wanazingatia muda wa utekelezaji kwa kukamilisha mapema na kwa ubora wa hali ya juu.
Kuhusiana na gharama za nyumba hizo Arch. Kondoro amesema, Serikali imetoa mwongozo wa kodi kwa ajili ya watumishi wa Umma ni theluthi mbili ya soko (kodi zinazotozwa mtaani.)
Awali msimamizi wa mradi huo Arch. Benard Mayemba amesema miradi ya Magomeni Kota Phase 2A na kuendelea na mradi wa Temeke Mwisho inatekelezwa kwa fedha za ruzuku na gharama za ujenzi katika eneo la Temeke Mwisho utagharimu Bilioni 17 hadi 19 na utachukuwa Kaya 148 na inategemewa kujengewa majengo 7 zaidi yatakayobeba Kaya 1000.