TBS YAENDELEA KUTOA ELIMU YA VIWANGO KWA WAZALISHAJI NA WAAGIZAJI WA BIDHAA NJE YA NCHI

 Maafisa wa TBS na ZBS wakitoa elimu ya namna ya kuthibitisha ubora wa bidhaa kwa mjasiriamali wakati wa Tamasha la tisa la Biashara visiwani Zanzibar. Afisa Masoko (TBS) Bi. Deborah Haule, akitoa elimu ya viwango kwa mzalishaji wa bidhaa wakati wa Tamasha la Tisa la Biashara visiwani Zanzibar.

**************************

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa elimu ya Viwango kwa wazalishaji, wasambazaji, waagizaji wa bidhaa nje ya nchi, wafanyabishara na wananchi kwa ujumla visiwani Zanzibar .

Elimu hiyo imetolewa wakati wa Tamasha la Tisa la Biashara Zanzibar linaloendelea katika Viwanja vya Maisara visiwani hapa. TBS inatoa elimu hiyo kutokana na mojawapo ya jukumu yake ni kutoa elimu kwa wananchi, wazalishaji na wafanyabiashara kwa ujumla, hivyo kuwepo katika maonesha hayo kunarahisisha utoaji huduma hiyo.

Akizungumza wakati wa Tamasha hilo jana Afisa Masoko wa TBS, Bi. Deborah Haule alisema shirika linatumia Tamasha hilo kutoa elimu kuhusu majukumu yake mengine ambayo ni pamoja na uthibitishaji wa bidhaa na mifumo, usajili wa majengo na bidhaa za chakula na vipodozi, upimaji, uandaaji wa viwango na udhibiti ubora kwa bidhaa zinazotoka nje ya nchi.

“TBS ni shirika lililopewa dhamana ya kusimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini na zile zinatoka nje ya nchi, hivyo basi wazalishaji, wasambazaji, waagizaji wa bidhaa nje ya nchi na wafanyabiashara wanatakiwa kuhakikisha bidhaa wanazozalisha na zile zinazotoka nje ya nchi zimethibishwa na kukidhi matakwa ya viwango kabla ya kuingizwa sokoni,” alisema Haule

Aliongeza kuwa wananchi kama watumiaji wa bidhaa wao wana nafasi kubwa ya kufanya kuhakikisha bidhaa zilipo sokoni zimekidhi matakwa ya viwango kwani wao ndio wanofanya maamuzi ya kununua au kutokununua bidhaa fulani.

“Wananchi kama watumiaji wa mwisho wa bidhaa ndio waathirika wakubwa wa bidhaa hafifu na endapo watajenga utamaduni wa kununua bidhaa zile tu ambazo zimethibitishwa ubora wake kwa hakika soko la Tanzania litajazwa na bidhaa zilizokidhi matakwa ya viwango tu na kwa pamoja kama Taifa tutakuwa tumeishinda vita ya bidhaa hafifu’ alisisitiza Bi. Haule na kuongeza:

“Jukumu la kuhakikisha Tanzania inakuwa na bidhaa zilizokidhi matakwa ya viwango si la TBS pekee yake, bali ni jukumu la kila Mtanzania kuanzia mzalishaji wa bidhaa, muagizaji wa bidhaa nje ya nchi,msambazaji wa bidhaa, muuzaji wa bidhaa na mtumiaji wa bidhaa. Hiyo basi tukiamua kwa pamoja tutajenga Taifa salama na kukuza uchumi wa nchi kwani bidhaa zetu zitakubalika katika masoko ya kitaifa na kimataifa

Post a Comment

Previous Post Next Post