DKT.JAFO APONGEZA WALIMU KUSIMAMIA UPANDAJI MITI

  

WAZIRI  wa Nchi Ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo,akizungumza  kwenye Mkutano wa 17 wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) uliofanyika jijini Dodoma.
 

WASHIRIKI wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo,(hayupo pichani) wakati wa  Mkutano wa 17 wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) uliofanyika jijini Dodoma.

………………………………
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewapongeza walimu wote nchini kwa kuipokea vizuri na kuitekeleza Kampeni ya Soma na Mti.
Ametoa pongezi hizo leo Desemba 16, 2022 wakati alipokaribishwa kuzungumza kwenye Mkutano wa 17 wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) uliofanyika jijini Dodoma.
Dkt. Jafo amesema kuwa kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi inayoikabili nchi yetu na dunia kwa ujumla bado tunao wajibu wa kuendelea kupanda miti ili kukabili athari hizo.
Kampeni hiyo aliyoizindua Januari 20, 2022 inahusisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo ambapo lengo lake ni kuwahamasisha kupanda miti kwa wingi katika maeneo yao.
Dkt. Jafo ametoa wito kwa walimu hao kuendeleza ajenda ya upandaji miti kwa kuhamasisha pia kwa wazazi wa wanafunzi wao na wananchi kwa ujumla kushiriki katika kampeni ya upandaji miti na usafi wa mazingira.
“Nilipozindua Kampeni ya ‘Soma na Mti’ hapa jijini Dodoma nikiwaomba walimu wote washiriki na hili nilifanya kwasababu nchi yetu ina wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zaidi milioni 14.1 na wale wa vyuo ni takriban laki nne hivyo makisio ya wanafunzi wote ni milioni 14 na laki tano idadi ambayo inaweza kutusaidia kupata miti kwa wingi,” amesema. 
  
Hivyo, Waziri Jafo amewashukuru na kuwapongeza kwa kuipokea vizuri kampeni hiyo huku akiwaomba kuwa mabalozi wazuri katika mitaa na vijiji wanakotoka kwa kuhamisha ajenda ya upandaji miti na usafi wa mazingira.
Kuhusu Biashara ya Kaboni waziri huyo amesema kwa shule zenye mashamba mbali ya kufaidika na mazao kama vile mikorosho pia inaweza kupata fursa ya kuvuna hewa ukaa na kuingiza kipato.

Post a Comment

Previous Post Next Post