Watendaji wa taasisi za Serikali wametakiwa kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia uanzishaji wa viwanda nchini.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaban, tarehe 4 Desemba, 2022 wakati akifungua rasmi Maonesho ya Saba ya Tanzania katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Shabaan amesema sekta ya viwanda ni nyezo muhimu ya kufanikisha malengo ya dira ya maendeleo ifikapo 2025 ya kufikia uchumi wa kati ya juu, hivyo mazingira wezeshi kwa maendeleo ya uwekezaji wa viwanda yatasaidia kufikia malengo hayo.
"Taasisi za Serikali zinapaswa kutekeleza ipasavyo mpango wa kuboresha mazingira ya biashara ili kuwezesha ukuaji wa sekta ya viwanda nchini", amefafanua Mhe.Shaaban.
Awali Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Ally Gugu akimkaribisha Waziri Shaaban wa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Ashatu Kijaji amewataka waandaaji na washiriki wa maonesho hayo kuhakikisha kuwa wanatekeleza kwa vitendo kwa kununua bidhaa za Tanzania ili kujenga Tanzania kama kauli mbiu ya maonesho hayo inavyoeleza.
Amesema fursa hii itumike pia kujitangaza sambamba na uzalishaji wa bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
Maonesho hayo ya bidhaa za Viwanda vya Tanzania yenye kauli mbiu ya "Nunua bidhaa ya Tanzania Jenga Tanzania #Nunua cha Kwetu" yameanza terehe 03 Desemba, 2022 na yatahitimishwa tarehe 09 Desemba, 2022 huku BRELA ikishiriki kikamilifu kutoa huduma za urasimishaji wa biashara.