Mwandishi wetu,Dar es Salaam
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kikodi Kariakoo, Bw. Alex Katundu amezindua kampeni ya twende nao tukawaelimishe yenye lengo la kuwaelimisha wanunuzi juu ya umuhimu wa kudai risiti za kielektroniki za EFD kila wanaponunua bidhaa katika eneo la kibiashara la Kariakoo.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa elimu ya umuhimu wa kudai risiti kwa wanunuzi waliokutwa wamenunua bidhaa bila kudai risiti, Meneja huyo ameeleza kuwa, elimu ya kodi imekuwa ikitolewa mara kwa mara kwa wafanyabiashara suala ambalo limesababisha wanunuzi wengi kusahau wajibu wao wa kudai risiti.
“Mara nyingi tumekuwa tukitoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu matumizi sahihi ya mashine za kutolea risiti za EFD na sasa hivi tumekuja na mkakati maalumu wa kuwaelimisha wanunuzi juu ya haki yao ya kudai risiti kila wanapofanya manunuzi,” alisema Meneja Katundu.
Alisema kuwa, zoezi hili litafanyika kwa kuwakusanya wanunuzi wote watakaokutwa wamenunua bidhaa bila kuwa na risiti na kupelekwa katika ofisi ya TRA Kariakoo iliyopo Mtaa wa Lumumba na Kipata, Dar es Salaam kwa ajili ya kuwaelimisha.
“Kwakuwa wanunuzi hawa wanakutwa katika maeneo mbalimbali ya Kariakoo, hivyo zoezi hili linafanyika kwa kuwakusanya wote wanaokutwa wamenunua bidhaa lakini hawana risiti ambapo wanaletwa hapa ofisini kwa ajili ya kuwaelimisha na kuwaomba wawe mabalozi kwa wengine wenye tabia ya kutokudai risiti,” alifafanua Katundu.
Alisema elimu hiyo itakuwa ikitolewa bure kwa kuwaeleza wanunuzi umuhimu wa kudai risiti ili kuepuka adhabu ya faini ya sh. 30,000 hadi sh. milioni 1.5.
Kwa upande wake mnunuzi wa bidhaa Kariakoo, Elizabeth Kimaro, alitoa wito kwa wanunuzi wenzake wenye tabia ya kutokudai risiti kutumia haki na wajibu wao wa kudai risiti kwa maendeleo ya Taifa.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kikodi Kariakoo Bw. Alex Katundu akizungumzia Kampeni ya Twende nao Tuwaelimishe yenye lengo la kutoa elimu kwa wanunuzi wa bidhaa mbalimbali juu ya umuhimu wa kudai risiti za EFD kila wanapofanya manunuzi. Kampeni hiyo imezinduliwa leo