MENEJIMENTI YA TAWA YATAKIWA KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO

  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb)ameitaka  menejimenti  Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ifanye kazi kwa ushirikiano ili kuiwezesha taasisi hiyo kutimiza malengo yaliyowekwa.

 Mhe. Mary Masanja ametoa kauli hiyo leo jijini Mwanza mara baada ya kuitembelea menejimenti ya TAWA inayoendelea na mafunzo ya uongozi  katika Chuo cha Usimamizi wa  Wanyamapori Pasiansi.

Amewaeleza kuwa utendaji kazi wenye kuzingatia  ushirikiano na Upendo ni nguzo muhimu itakayowawezesha  kurekebishana na kukosoana kiutendaji  kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Aidha, amesisitiza kuwa ni vyema menejimenti hiyo ikajiwekea utaratibu wa kujadili changamoto mbalimbali pamoja ili iweze  kufika mbali kiutendaji.

"Mwenzako anapokutana na changamoto yoyote ichukulie kama ni yako. Tunahitaji  tufanikiwe kwa kutatua changamoto zinazotukabili kwa pamoja " amesisitiza Mhe. Masanja.

Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo viongozi  katika usimamizi wa masuala mbalimbali yakiwemo ya rasilimali watu, fedha na taratibu za manunuzi yametolewa kwa Manaibu Kamishna, Makamanda wa Kanda, Makamishna Wasaidizi Wandamizi na Makamishna Wasaidizi




Post a Comment

Previous Post Next Post