JAFO AZINDUA JOSHO SIMANJIRO

  Waziri Jafo azindua josho Simanjiro kupitia Mradi wa EBARR

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt.
Selemani Jafo amezindua josho la kuogeshea mifugo katika Kijiji cha Irkujit
wilayani Simanjiro mkoani Manyara ambalo limejengwa kupitia Mradi wa Kuhimili
Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).

Akizungumza na wananchi wakati wa ziara ya kukagua mradi huo Desemba 15,
2022 amewapongeza wananchi hao kwa kuibua mradi huo ambao
unawawezesha kuikinga mifugo yao kwa magonjwa yaenezwayo na kupe na
mbung’o.

Dkt. Jafo amesema josho hilo linalotarajiwa kuhudumia wananchi takriban
30,000 wa kijiji hicho na vijiji jirani ni matunda ya Serikali katika kuhakikisha
inawasidia wananchi kupambana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Alisema athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa zinazosababisha maeneo ya
nchi kuwa na ukame ambao ni chanzo cha kukosekana kwa mvua, hivyo
matokeo yake ni kukauka kwa vyanzo vya maji vikiwemo mabwawa.

“Ndugu zangu leo hii ukienda Mto Ruaha ambao ndio chanzo cha maji
kinachopeleka katika Bwawa la Mtera umekauka, pia Kidatu maji yamepungua na
ndio maana tumeshuhudia baadhi ya maeneo yanapata mgao wa umeme, hayo
yote ni mabadiiko ya tabianchi,” amesema Dkt. Jafo.

Aliweka bayana kuwa ili kukabiliana na changamoto kama hizo, Ofisi ya Makamu
wa Rais inatekeleza Mradi wa EBARR katika baadhi ya vijiji ambavyo vinakabiliwa
na changamoto ya ukame ili kuwasaidia wananchi wa maeneo hayo.

Waziri huyo ameupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa kuisimamia mradi hiyo
katika eneo lao huku akitoa rai kwa wananchi wa Wilaya ya Simanjiro kuitunza ili
isiharibiwe na idumu kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Katika ziara hiyo pia alitembelea na kukagua miradi mingine ikiwemo wa kikundi
cha uzalishaji wa bidhaa za ngozi na ujenzi wa bwawa linalotarajiwa kusaidia
upatikanaji wa maji ambao unaendelea kutekelezwa kupitia EBARR.

Hata hivyo ameonesha kutoridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wake ambao
ameelekeza watalaamu ngazi ya wilaya wanaousimamia wahakikishe
unarekebishwa dosari zote zilizojitokeza na kukamilika kwa wakati ili kuendana
na thamani ya fedha iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi huo.

Kutokana na kuchelewa kukamilika kwa mradi huo Waziri Jafo amemuelekeza
mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kuukamilisha ifikapo Januari 15, 2023 ili uanze
kuhudumia maelfu ya wananchi wa kijiji hicho ikiwa ni hatua ya Serikali ya
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dk. Suleiman Serera
ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ujumla kwa kupelekea mradi huo
wilayani humo ambako kuna changamoto ya ukame.

Amesema ni dhahiri kuwa kazi inaonekana kupitia katika shughuli mbalimbali
zinazofanywa na wanavikundi vikiwemo ufugaji wa nyuki ambao wanatumia
misitu iliyofadhiwa.

Aidha, Dkt. Serera ameiomba Ofisi ya Makamu wa Rais kupanua wigo wa mradi
huo katika maeneo mengine kwa kuwa wafugaji wengi wanahitaji majosho ya
kuogeshea mifugo ili kukabiliana na athari za maabdiliko ya tabianchi.

Wakizungumza kwa niaba ya wananchi Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mhe.
Christopher Ole Sendeka na Diwani wa Kata ya Irujit pia wamepongeza juhudi za
Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wilayani humo.

Viongozi hao wawili pia watumia nafasi hiyo kutoa wito kwa Ofisi ya Makamu wa
Rais kuongeza vijiji katika utekelezaji wa mradi huo ili wananchi wengi zaidi
wafaidike nao.

Katika ziara ya hiyo Waziri Dkt. Jafo amepewa heshima ya Laigwanani na Jamii
ya Wamasai kutoka Wilaya ya Simanjiro.

Mradi wa EBARR unatekelezwa pia katika wilaya za Mpwapwa (Dodoma),
Mvomero (Morogoro), Kishapu (Shinyanga) na Kaskazini ‘A’ iliyopo Mkoa wa
Kaskazini (Zanzibar).

 

Post a Comment

Previous Post Next Post