**********
NA MWANDISHI WETU
Serikali ya Tanzania imeikabidhi Burundi kiti cha uenyekiti wa Mawaziri waliopo katika Mkataba swa Kikanda wa Usimamizi Endelevu wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika na kusisitiza Kiswahili kitumike kama lugha kuu ya mawasiliano katika mikutano yote itakayofanyika.
Hayo yamejiri wakati wa Mkutano wa 10 wa Mawaziri hao uliofanyika jana jijini Bujumbura nchini Burundi baada ya Tanzania kumaliza muda wa uenyekiti uliodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo kwa Waziri wa Mazingira, Kilimo na Mifugo wa Burundi Prof. Sanctus Niragira, alisema Tanzania inashiriki katika shughuli zote zinazolenga kuhakikisha usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa hilo.
Pia, alisema Tanzania imedhamiria kushirikiana na nchi wanachama ambazo ni Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Jamhuri ya Zambia katika utekelezaji wa programu za kikanda zinazolenga kulinda rasilimali za pamoja za Ziwa Tanganyika na kuboresha maisha ya watu katika ukanda huo.
Dkt. Jafo alisema Ziwa Tanganyika ni rasilimali muhimu kwa wananchi takriban milioni 10 wa ukanda huo wanaolizunguka hivyo zinahitajika juhudi za pamoja katika kulilinda.
“Waheshimiwa mawaziri, mazingira tunayoishi yanabadilika haraka sana na shughuli za binadamu zinatumia maliasili za dunia kwa kasi ya kutisha na kuharibu mifumo ikolojia.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya viumbe 22,000 wako hatarini kutoweka ikiwa ni pamoja na baadhi ya viumbe katika Ziwa Tanganyika,” alisema.
Hivyo, alitoa wito kwa Mawaziri hao kutoka nchi wanachama kuungana kwa pamoja kujadili namna bora ya kulinda Ziwa Tanganyika kwa manufaa ya kizazi cha leo na kizazi kijacho huku akisisitiza umuhimu wa kuweka utaratibu wa muda mrefu wa ufadhili wa programu ya maendeleo ya Ukanda ya Ziwa Tanganyika.
Aidha Mkutano huo wa nchi wanachama wa Mkataba wa hifadhi na Usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika ulifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Prosper Bazombanza.