Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti Bi.Happiness Mbelle akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea leo mkoani Morogogo
Washiriki wa mafunzo ya wakaguzi mbolea wakifuatilia kwa makini mada kuhusu Sheria ya Mbolea na kanuni zake iliyowasilishwa na Kaimu Meneja Huduma za Sheria Bi. Belinda Kyesi ( hayupo pichani)
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi Fatma Mwasa (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya wakaguzi wa mbolea baada ya kufungua mafunzo hayo leo tarehe 14.11.2022 mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bi.Fatma Mwasa ametoa wito kwa maafisa ugani nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Bi Mwasa ametoa wito huo leo tarehe 14.11.2022 mkoani Morogoro alipokuwa akifungua mafunzo ya wakaguzi wa mbolea yanayofanyika kwa siku tano katika ukumbi wa idara ya misitu.
Mkuu wa Mkoa huyo amesema ipo haja kwa wataalamu wa kilimo kuendelea kutoa elimu kwa wakulima nchini ili matumizi ya mbolea yaongezeke na kuwawezesha kupata mazao mengi katika eneo dogo.
Amesema inasikitisha kuona kuwa wakulima wengi nchini wanatumia nguvu na raslimali nyingi kulima eneo kubwa lakini tija ni ndogo sana.
"Wakulima wetu bado wanaona ni fahari kulima eneo kubwa bila kujali tija inayopatikana" Alisema Mwasa.
Mwasa aliongeza kuwa matumizi sahihi ya mbolea yatawasaidia wakulima kuzalisha ziada ya mazao ya chakula na hivyo kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Aidha, Bi. Mwasa amewataka washiriki wa mafunzo ya ukaguzi wa mbolea kuzingatia watakayofundishwa kwani ndio msingi wa kuwa na mbolea yenye ubora nchini.
Akizungumza awali kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji TFRA Bi. Happiness Mbelle alisema jukumu kubwa la TFRA ni kuhakikisha kuwa mbolea yenye ubora inawafikia wakulima kwa wakati na kwa bei himilivu.
Bi.Mbelle amesema katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 Mamlaka imepewa jukumu la kusimamia mpango wa utoaji wa mbolea za ruzuku ambapo
wakaguzi wa mbolea wanatakiwa kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea yenye ubora na viwango vinavyokubalika.
Mafunzo hayo yamewaleta pamoja maafisa ugani wapatao 30 kutoka katika mikoa 19 nchini ambao watapewa vyeti vya kuwa wakaguzi wa mbolea na kisha kuchapishwa katika gazeti la serikali.
Hadi sasa, TFRA imetoa mafunzo kwa wakaguzi wa mbolea zaidi ya 140 nchini.