****************
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wafanyabiashara na watoa huduma wakubwa na wadogo kuchangamkia fursa ya kushiriki Tuzo za ubora kwenye huduma na bidhaa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 11,2022 Jijini Dar es Salaam,Afisa Udhibiti Ubora TBS, Bw. Baraka Mbajije amesema lengo la Tuzo hizo ni kuhakikisha kuwa mifumo ya bidhaa na huduma zinakidhi ubora kitaifa, kikanda na kimataifa na hivyo kufanya vizuri kwenye masoko ya ngazi zote.
Aidha Bw.Mbajije amesema "tuzo hizi ni sehemu ya mipango ya serikali katika kuboresha huduma na bidhaa zinazotengenezwa nchini kupitia matumizi ya viwango na kanuni za ubora kwa taasisi za umma na binafsi"
Kwa upande wake Afisa Viwango TBS, Bw. Salim Mohamed amesema tuzo hizo zimegawanyika katika vipengele vitano ambavyo ni:-
▶️Tuzo kwa kampuni bora ya mwaka,
▶️ Tuzo kwa bidhaa bora ya mwaka,
▶️ Tuzo huduma bora ya mwaka,
▶️ Tuzo kwa muuzaji bora wa bidhaa nje ya nchi
▶️ Tuzo ya mtu mmoja mmoja aliyefanya vizuri kwenye masuala ya ubora.
“Kwa kipengele cha kwanza hadi cha nne zimeandaliwa tuzo kwenye makundi mawili kwa kila kipengele yaani tuzo kwa kampuni kubwa na pia tuzo kwa wajasiriamali wadogo na wakati" - ndugu Salim Mohamed Ameyasema hayo katika Mkutano na Waandishi wa habari
Bw. Mohamed amesema wadau wote wanaotaka kushiriki basi watembele katika tovuti rasmi ya TBS ( www.tbs.go.tz) watakuta link ya Jinsi ya kushiriki na Mwisho wa kutuma Maombi ni Tarehe 17 NOVEMBA, 2022