PROGRAMU YA UCHUMI WA BLUU KUCHOCHEA UPATIKANA FEDHA ZA MABADILIKO YA TABIANCHI

  

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akishiriki uzinduzi wa Programu ya Utekelezaji wa Uchumi wa Bluu kwa nchi za Kiafrika ikiwemo Tanzania kupitia Benki ya Dunia uliofanywa wakati Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) unaofanyika Sharm El Sheikh, Misri.

………………………………

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema kuanzishwa kwa Programu ya Uchumi wa Bluu kwa Afrika itachochea upatikanaji wa fedha za kusaidia katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabanchi.

Pia, amesema Serikali imejumuisha masuala ya hifadhi ya mazingira katika Uchumi wa Bluu ili kuhakikisha unakuwa endelevu kwa manufaa ya jamii ya Tanzania.

Mhe. Khamis amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Programu ya Utekelezaji wa Uchumi wa Bluu kwa nchi za Kiafrika ikiwemo Tanzania kupitia Benki ya Dunia uliofanywa wakati Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) unaofanyika Sharm El Sheikh, Misri.

Alisema kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na ukanda wa pwani wenye urefu wa takriban kilomita 1,450 kwa urefu ambao unatoa fursa kwa wananchi kujishughulisha na shughuli za uchumi wa bluu kwa vitendo zikiwemo uvuvi.

Naibu Waziri Khamis alisema kuwa eneo hilo linachukua takriban asilimia 15 ya ardhi yote ya Tanzania ambapo takriban watu milioni nane wananufaika nalo hivyo, Serikali imeweka utaratibu wa kusaidia utekelezaji wa ajenda ya uchumi wa bluu.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni kuanzishwa kwa Wizara Maalum ya Uchumi wa Bluu Zanzibar, kuanzisha Sera na Mkakati wa Maendeleo Uchumi wa Bluu Zanzibar na Mkakati wa Uchumi wa Bluu Tanzania Bara.

“Uchumi wa bluu unatarajiwa kuchochea matumizi makubwa ya rasilimali za maji na maeneo ya pwani, hata hivyo, changamoto za kimazingira zinazosababisha mabadiliko ya tabianchi na uvuvi haramu huenda zikahatarisha au kudhoofisha matarajio ya ukuaji wa uchumi wa bluu,” alisema.

Pia, aliishukuru Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi Mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) ambao umesaidia kutokomeza vitendo vya uvuvi haramu.

Naibu Waziri Khamis aliongeza kuwa mradi huo umesaidia na kuimarishwa kwa ulinzi wa makazi ya samaki na matumbawe ya baharini ambapo awali kulifanyika uvuvi haramu uliochangia uharibifu wa makazi na viumbe hai.

Post a Comment

Previous Post Next Post