MWANDISHI SELEMANI MSUYA AZOA TUZO COSTECH

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga akimkabidhi cheti cha ushindi wa Mwandishi Bora wa Makala za Bioteknolojia zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu

 Na Mwandishi Wetu

MWANDISHI Mwandamizi wa Gazeti la Raia Mwema, Selemani Msuya amekomba tuzo za mwandishi bora wa mwaka 2022 zinazilizotolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Msuya ametwaa tuzo mbili ambapo ya kwanza ni Tuzo ya Mwandishi Bora wa Makala za Bioteknolojia na Tuzo ya ya Mshindi wa Jumla.

Msuya ametwaa tuzo hizo baada ya kuandika makala mbalimbali zinazohusiana na masuala ya bioteknolojia na uhandisi jeni ambapo alishiriki na waandishi wa vyombo vingine vya habari na kuibuka mshindi wa jumla.

Mwandishi Lucy Ngowi wa Gazeti la Habari Leo, ametwaa Tuzo ya Habari za Sayansi kwa Lugha  ya Kiswahili na Tuzo ya Mwandishi wa Habari za Sayansi wa wakati wote.

Naye Mwandishi Benson Eustace wa Azam TV amekuwa mshindi wa Bora wa Vipindi vya Sayansi baada ya kuandaa vipindi mbalimbali.

Msuya na Benson pamoja na kushinda tuzo hizo katika ngazi ya nchi wamechaguliwa kushiriki shindano la mwandishi bora wa habari za bioteknolojia na sayansi Afrika ambazo zinafanyika jijini Abuja nchini Nigeria Desemba 2,2022.

Akizungumza baada ya kutoa tuzo hizo, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu alisema wametoa tuzo na zawadi kwa waandishi wanaondika habari za sayansi, ubunifu na bioteknolojia ili kuchochea uandishi wa habari unaogusa jamii.

Alisema pia COSTECH kwa kushirikiana na wadau wengine imekuwa ikitoa tuzo mbalimbali kwa vijana wabunifu wa teknolojia mbalimbali, hali ambayo inaongeza kasi ya ubunifu nchini.

“Tumetoa tuzo za vyeti na zawadi kidogo kwa waandishi wa habari watatu ambao wameandika habari za sayansi, ubunifu na bioteknolojia. Tunawasihi waandishi kuandika habari hizi kila mwaka tutaendelea kuwatambua,” alisema.

Naye Naibu Waziri Kipanga alisema Serikali itaendelea kuwezesha na kusaidia vijana wabunifu katika eneo lolote ambalo litaweza kuleta tija kwenye kuchochea maendeleo ya nchi.

Alisema katika kipindi hiki Serikali pamoja na wadau mbalimbali wametoa zaidi ya Sh.bilioni 1.1 kwa vijana wabunifu, waweze kuendeleza bunifu zao.

“Katika bajeti ya 2022/2023 Serikali ilitenga Sh.milioni 700, lakini wadau wa maendeleo kama SIDA wametoa zaidi ya Sh.milioni 450 katika eneo hilo la ubunifu,” alisema.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha bunifu ambazo zinabuniwa zinaenda sokoni kutatua changamoto ambazo zinakabili jamii.

Naibu Waziri Kipanga alitoa wito kwa wadau wa maendeleo wakiwemo Benki ya CRDB, NMB, Ufunguo na wengine kujitokeza ili kuwezesha wabunifu ambao wamekuwa wakibuni teknolojia zinazoenda kutatua changamoto za jamii.

Mwisho

Post a Comment

Previous Post Next Post