Airtel yashirikiana na COSTECH kuandaa shindano la kompyuta na ubunifu
Dar es Salaam Jumapili 27 Novemba 2022 Kampuni ya mawasiliano ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) wameendesha mashindano ya ubunifu kwa vijana yenye lengo la kutoa elimu juu ya njia mbalimbali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira kupitia ubunifu wa sayansi na teknolojia
Mashindano hayo yalishirikisha wanafunzi kutoka shule mbalimbali nchini ambapo waliwasilisha miradi mbalimbali ya michezo ya video yenye njia mbalimbali za kuzuia na kupambana uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kupunguza ukataji wa miti, utunzaji wa vyanzo vya maji, kupunguza uzalishaji wa huwa ya ukaa na vilevile kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa mashindano hayo Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi kutoka COSTECH Emmanuel Mgonja ameweka wazi kuwa ubunifu wa sayansi na teknolojia unamchango mkubwa katika kutatua changamoto za ajira nchini hivyo amewataka walimu na wanafunzi waliopata elimu hiyo kujikita katika kutanua wigo wa ujuzi kwa jamii inayowazunguka
Kwa upande wake meneja uhusiano wa kampuni ya Airtel Tanzania Jackson Mbando ameeleza kuwa wamejipanga kikamilifu kihakikisha kuwa vijana wanajengewa uwezo wa kutumia vifaa mbalimbali vya kidigitali katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii hatua itakayosaidia kuongeza ushiriki wa vijana kwenye kuleta maendeleo endelevu katika jamii
Nao baadhi ya wanafunzi walioshiriki mashindano hayo wamewashukuru waandaaji wake na kuwataka wadau mbalimbali wa maendeleo kuunga mkono juhudi hizo ili kutoa fursa kwa wanafunzi wengi zaidi kupata elimu hiyo na kuweza kutambua fursa mbalimbali za kimaendeleo zinazotokana na ubunifu wa sayansi na teknolojia.