Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza katika uzinduzi wa Mpango Mkakati wa kusimamia Mazingira katika Ziwa Victoria.Uzinduzi huo umefanyika leo Julai 13,2022 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka akizungumza katika uzinduzi wa Mpango Mkakati wa kusimamia Mazingira katika Ziwa Victoria. Uzinduzi huo umefanyika leo Julai 13,2022 Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa CSE, Dkt. Sunita Narain akizungumza katika uzinduzi wa Mpango Mkakati wa kusimamia Mazingira katika Ziwa Victoria. Uzinduzi huo umefanyika leo Julai 13,2022 Jijini Dar es Salaam.
**************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema kuimirika kwa usafi wa mazingira kunapunguza kwa kiasi kikubwa mlipuko wa magonjwa mbalimbali hivyo wananchi kwa ujumla wanajukumu la kulinda na kutunza mazingira katika maeneo yanayowazunguka.
Ameyasema hayo leo Julai 13,2022 Jijini Dar es Salaam wakati akizindua Mpango Mkakati wa kusimamia Mazingira katika Ziwa Victoria.
Mpango huo unaratibiwa na Kituo cha Sayansi ya Mazingira Center for Science Environment (CSE) cha nchini India ambacho kimekuwa kikitafiti chanzo cha uchafuzi wa ziwa hilo na kutafuta majibu yake.
Amesema Serikali inataka kuona hali ya usafi katika ziwa victoria inakuwa endelevu katika kipindi chote hata katika kipindi cha msimu wa mvua na kuwafanya wadau kuvutika zaidi.
Aidha Waziri Jafo amesema ziwa Victoria limekuwa chanzo kikubwa cha maji ya Mto Nile ambao unategemewa na zaidi ya watu milioni 40 kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kilimo na uvuvi.
“Hili ziwa ni kubwa sana na linategemewa zaidi duniani kwasababu maji yake ndiyo uchumi wa wenzetu kwa hiyo ninapoona wadau kama nyinyi mnajitokeza kulilinda inanipa moyo sana, wenzetu Misri wanategemea sana mto Nile ambao unapata maji kupitia ziwa Victoria, ” Amesema Waziri Jafo.
Pamoja na hayo Waziri Jafo amepongeza ushirikiano mwema uliopo baina ya serikali ya Tanzania na India ambayo alisema kwa sasa inafadhili miradi 28 ya maji yenye thamani ya zaidi ya trilioni moja kwenye mikoa mbalimbali nchini na tayari imeshaanza kujengwa.
“Serikali ya India inatusaidia sana kwenye mambo mengi sasa ninapoona na nyinyi mmekuja kutusaidia kulinda ziwa Victoria dhidi ya uchafuzi wa mazingira yake inazidi kunipa amani ya moyo kwamba nyinyi ni ndugu zetu na mnapenda maendeleo yetu,” Amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Samuel Gwamaka, amesema Baraza lipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika shughuli za uhifadhi wa mazingira nchini.
Amesema wanashirikiana katika kuandaa shughuli mbalimbali za kimazingira ikiwa ni pamoja na uandaaji wa Mpango Mkakati wa Usimamizi wa Mazingira kwa Ziwa Victoria na kwamba uandaaji wa mpango huo umezingatia miongozo mbalimbali ya nchi.
“Uanzishaji wa mkakati huu ni jitihada za Baraza katika utekelezaji wa Mkakati Kabambe wa Mazingira wa Taifa wa Mwaka 2022/32 uliozinduliwa rasmi mwezi Juni 2022 na pia Ajenda ya Taifa ya Tafiti za Mazingira (2017/22),” Amesema Dkt.Gwamaka.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CSE, Dkt. Sunita Narain, alipongeza jitihada zinazofanywa na serikali kulinda na kuhifadhi mazingira na kwa namna ambavyo kituo hicho kimepata mapokezi mazuri.
“Tunaishukuru serikali ya Tanzania kwa kutupokea vizuri tangu tulipofika nchini mwezi uliopita, tumetembelea ziwa Victoria kujionea hali ilivyo na tumeridhika kwa namna mikakati inavyowekwa kulilinda dhidi ya uchafuzi,” Amesema Dkt. Suniti