No title

 Na Mary Gwera, Mahakama

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuweka bayana taarifa za ardhi na makazi kwa wananchi ili kuepuka ongezeko la migogoro ya ardhi nchini.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi leo tarehe 13 Julai, 2022 jijini Dar es Salaam alipokuwa kwenye ziara ya kikazi katika Divisheni hiyo, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, migogoro mingi ya ardhi inatokana na kutokuwa na taarifa sahihi za umiliki wa ardhi hali inayosababisha wananchi kuwa na migogoro ya ardhi ya mmiliki halali wa eneo husika.

“Pengine imefika wakati sasa taarifa zinazokusanywa na Wizara husika ziweze kupatikana kwa wananchi ili masuala ya ardhi yaweze kuwa wazi zaidi na yasiibue migogoro ambayo inachukua muda mrefu mahakamani,” amesema Jaji Mkuu.

Aidha, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma amebainisha juu ya umuhimu wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi kuangalia pia uwezekano wa kutumia Usuluhishi kama njia mojawapo ya kupunguza mlundikano wa mashauri ya Ardhi.

“Jambo lingine la kuangalia katika kupunguza migogoro ya ardhi ni suala la Usuluhishi, inabidi kuangalia uwezekano wa mashauri ya ardhi yaishie kwenye hatua ya usuluhishi ili yasichukue muda mrefu mahakamani,” ameongeza Mhe. Prof. Juma.

Ameongeza kuwa, ni muhimu Majaji kuisoma Sheria ya Usuluhishi ya mwaka 2020 (Arbitration Act, 2020) ili kuangalia maeneo ambayo yanaweza kusaidia kupungua mashauri ya migogoro ya ardhi kwa njia ya usuluhishi, huku akiwasisitiza pia kutotumia kwa wingi vigezo vya kiufundi katika uendeshaji wa mashauri hayo ili kuondokana na kadhia ya mlundikano.

Jaji Mkuu ametoa mfano wa baadhi ya nchi ambazo zinatumia njia ya usuluhishi katika utatuzi wa mashauri mbalimbali kuwa ni pamoja na Singapore ambayo inatumia njia hiyo kwa asilimia 90 huku Marekani ikiwa na asilimia 60 katika matumizi ya usuluhishi. Ameongeza kuwa, njia hii husaidia pia kuleta amani na kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa amesema Divisheni hiyo imejipanga thabiti kuondoa mlundikano wa mashauri, akieleza kuwa, kuanzia mwezi Januari mwaka huu mpaka sasa jumla ya mashauri 914 yamefunguliwa katika Divisheni hiyo huku mpaka sasa Divisheni hiyo imesikiliza na kuamua jumla ya mashauri 1,271 (ikiwemo sehemu ya mashauri yaliyosalia kwa mwaka jana).

“Mahakama ya Ardhi imejipanga kwa dhati, kuondokana na mlundikano, na hii ni kutokana na uwajibikaji pamoja na ushirikiano wa dhati wa Majaji wa Divisheni hii, napenda kuahidi leo kuwa mpaka kufikia mwezi Novemba mwaka huu tutakuwa hatuna mlundikano,” amesema Jaji Agnes.

Ameongeza kuwa, kwa mwaka 2021, Divisheni hiyo ilikuwa na mashauri yaliyobaki (pending cases) 2,246, mashauri yaliyofunguliwa (filed cases) 1,784 na mashauri yaliyoamuliwa (decided cases) yalikuwa 2,229.

Post a Comment

Previous Post Next Post