Serikali Kuendelea Kuimarisha TAWOMA Nchini, Kuwaondoa Wanawake Katika Umasikini

 

Mkurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza cha bodi mpya ya Chama cha wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. STAMICO ni mlezi wa chama hicho.
Mwenyekiti wa Chama cha wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Bi. Semeni Malale (wa pili kulia) akiteta jambo na viongozi wengine wa chama hicho: Katibu Mkuu, Bi. Salma Ernest (Kushoto), Makamu Mwenyekiti, Bi. Rachel Njau (wa pili kushoto) na kiongozi wa kamati ya Fedha na Uchumi ya chama, Bi. Hilda Jackson (kulia) wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza cha bodi mpya ya TAWOMA kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Migodi wa shirika hilo, Bw. Mbaraka Harun akizungumza wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza cha bodi mpya ya Chama cha wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam Kushoto ni Afisa Uhusiano wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Bi. Bibiana Ndumbaro.
Mwenyekiti wa bodi mpya ya Chama cha wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA), Mhandisi Dkt. Karim Baruti alipitishwa kwa kauli moja kuendelea kuongoza bodi hiyo kwa miaka mingine mitano wakati wa kikao hicho.
Mh. Ritha Kabati (Mb) ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya Chama cha wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) akichangia jambo wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza cha bodi mpya ya Chama cha wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) kilichofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. Wengine ni wajumbe wengine wa bodi hiyo: Mh. Bupe Mwakangata (Mb), kushoto na Dkt. Winnie Samwel (kulia).

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
SERIKALI imesema itaendelea kukisaidia Chama cha Wanawake Wachimbaji wa Madini Tanzania (TAWOMA) kuweza kufikia malengo yake ya kuwaendeleza na kuwawezesha wanawake walio katika mnyororo wa thamani wa Madini ili kuwakomboa na kuwaondoa kwenye Umasikini na kuongeza pato la Taifa.

Ahadi hiyo imetolewa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambalo ni mlezi wa chama hicho chenye wanachama zaidi ya 2,000 nchini wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza cha bodi mpya ya chama hicho mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

“Hatutawaacha,” aliahidi Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse aliyekuwa mgeni rasmi katika kikao hicho. Aliwapongeza wajumbe wa bodi hiyo mpya akisema wao ndio wabeba maono ya chama na kuwahimiza kutumia utaalamu na uzoefu wao kuhakikisha chama kinasonga mbele kwa maslahi makubwa ya wanawake wachimbaji madini na taifa kwa ujumla.

wanawake wachimbaji madini na taifa kwa ujumla.

Wajumbe wa kikao hicho walimpitisha kwa kauli moja Mhandisi Dkt. Karim Baruti kuendelea kuwa Mwenyekiti wa bodi ya TAWOMA kwa miaka mingine mitano. Wajumbe wa bodi hiyo ni pamoja na Dkt. Winnie Samwel, Bi. Hannah Kamau, Bw. Ibrahimu Shineni, Dkt. Hawa Mshana, Mh. Ritha Kabati (Mb) na Mh. Bupe Mwakangata (Mb).

Dkt. Mwasse alisema kutokana na utafiti uliofanywa na STAMICO kwenye sekta ya uchimbaji mdogo ilionekana matatizo makubwa manne yanayowakabili wachimbaji wadogo ni: ukosefu wa elimu ya uchimbaji, teknolojia duni isiyozingatia usalama na mazingira, ukosefu wa taarifa sahihi za mashapo hali inayosababisha kuchimba kwa kubahatisha na hivyo kutoaminika na kutokukopesheka.

“Changamoto hizo zinapelekea wachimbaji wadogo wakiwemo TAWOMA kutofaidika na raslimali za taifa kama inavyotakiwa na hii haina afya kwa taifa,” alisema.

Tayari hatua kadhaa zimeshachukuliwa ili kutatua changamoto hizo ikiwa ni pamoja na kutayarishwa kwa muongozo wa elimu utakaoanza kufanyiwa kazi mwaka huu wa fedha, kufungua vituo vya mafunzo ambapo wachimbaji wanajifunza kwa kuelezwa, kuona na kwa vitendo, kurahisisha upatikanaji wa taarifa za mashapo kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia Tanzania.

“Kwa kuanzia, tumeagiza mashine tano za kuchorongea maalumu kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambazo zitawekwa katika maeneo mbalimbali,” alisema na kuongeza kuwa gharama za kuchoronga na utafiti zikishuka, itasaidia kuwanyanyua wachimbaji wadogo na kukuza sekta ya madini kwa ujumla.

Kuhusu kukopesheka, tayari STAMICO imeshafikia makubaliano na taasisi kadhaa za fedha ili kurahisisha utoaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo. Alisema STAMICO itaendelea kuwatafutia masoko wachimbaji wanawake pamoja na wawekezaji wanaoweza kuwekeza katika maeneo yao ya uchimbaji.

“Nauona mwanga kwa TAWOMA. Mshikamano, upendo na kufanya kazi kwa pamoja ni muhimu ili kufanikisha malengo mliyojiwekea,” alishauri Dkt. Mwasse.

Akitoa salamu zake, Mwenyekiti wa bodi, Dkt. Baruti aliwashukuru wajumbe kwa kuwa na imani naye na kumpitisha tena kuongoza bodi hiyo. Alisema bodi itatumia uwezo wake wote kuhakikisha chama kinasonga mbele.

Kwa upande wake, Bi. Bertha Luzabiko, kamishna Msaidizi-Uongezaji Thamani Madini, Wizara ya Madini alisema Waziri wa Madini, Dkt. Dotto Biteko na Wizara yote kwa ujumla wana nia ya kuhakikisha wanawake wanaimarika katika mnyororo wa thamani wa madini na kuchangia pato la taifa zaidi.

“Mnao uwezo wa kuwa wachimbaji wa kati na wakubwa. Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi na rafiki kuwawezesha wachimbaji wadogo wote kufanya vizuri,” alisema Bi. Bertha na kusisitiza ushirikishwaji wa vijana.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa chama hicho mbele ya wajumbe wa mkutano, Katibu Mkuu wa TAWOMA, Bi. Salma Ernest alisema mikakati ya chama ni kuhakikisha kinaunganisha wanawake wote walio kwenye mnyororo wa thamani wa madini ili kuwa na sauti moja katika kujiletea maendeleo.

Mwenyetiti wa chama hicho, Bi. Semeni Malale aliwaambia waandishi wa habari kuwa dhana ya kuwa jinsia ya kike ni dhaifu na hivyo kutoweza kufanya kazi kama wachimbaji madini ni potofu kwa mazingira na dunia ya sasa.

“Utendaji wa wanachama wa chama hiki katika sekta ya madini ni uthibitisho tosha kuwa wanawake wanaweza,” alisema na kuhamasisha wanawake nchini kujiunga na sekta hiyo yenye fursa nyingi.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wawakilishi wa wadau wa TAWOMA kama benki ya NMB, shirikisho la sekta binafsi Tanzania (TPSF), shirika la PACT Tanzania na wabunge, Mh. Ritha Kabati na Mh. Bupe Mwakangata ambao ni mabalozi wa wanawake wachimbaji madini bungeni.

Post a Comment

Previous Post Next Post