Mhe. Mchengerwa Aeleza Umuhimu wa Kuwekeza katika Michezo

Na Mwandishi wetu, Birmingham

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa ameeleza kuwa, uwekezaji  katika michezo ni muhimu kwa kuwa unasaidia kutoa ajira na kukuza uchumi wa nchi.

Mhe. Mchengerwa ameeleza hayo leo Julai 27, 2022 katika Mkutano wa Mawaziri wa Michezo wa Nchi za Jumuiya ya Madola unaofanyika Birmingham Uingereza, ambapo amesema ni wakati sasa kwa nchi zinazoendelea kutoa kipaumbele katika michezo kama zinazofanya katika Sekta zingine.

"Ni wakati sasa wa kuipa Sekta ya michezo kipaumbele, tuondoe dhana ya kuchagua ikiwa tunataka kujenga miundombinu ya michezo na afya tunachagua afya, bali michezo pia tuipe kipaumbele kwakua katika Dunia ya leo,   michezo ni Sekta ambayo inatoa ajira na kukuza pato la nchi" alisema Mhe.Mchengerwa.

Ameongeza kuwa, ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi utasaidia Sekta hiyo kukua zaidi, huku akiwakaribisha wanachama wa Jumuiya hiyo kuwekeza katika michezo nchini Tanzania.


Mhe. Mchengerwa ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa, Tanzania imepiga hatua katika michezo ndani na nje ya nchi, ambapo timu mbalimbali  na wachezaji mmoja mmoja wamefanya vizuri.

Amesema katika Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan Tanzania imefanikiwa kufuzu  Kombe la Dunia kwa baadhi ya michezo, ikiwemo mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake chini ya Umri wa miaka 17 ambao wamefuzu kucheza Kombe la Dunia mwezi Oktoba, 2022, nchini India.

Ametaja pia Timu ya Walemavu ya  Tembo Worriors ambao wamefuzu Kucheza Kombe la Dunia mwezi Oktoba mwaka huu nchini Uturuki, pamoja na Timu mbili za mchezo  wa Kabbadi ambazo  zimefuzu kucheza  Kombe la Dunia mwezi Novemba 2022.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema Tanzania inajipanga kuwa mwenyeji wa mashindano ya Africa Cup of Nation ( AFCON) kwa wanawake mwaka 2024, na yale ya mwaka 2027, ambapo amewakaribisha wanachama wa Jumuiya hiyo kuunga mkono Tanzania.

Jumla ya wanamichezo 7,000 toka nchi 56 wanashiriki michuano hiyo katika jiji la Birmingham nchini Uingereza.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post