TAARIFA ZA WAMILIKI MANUFAA NI KIGEZO CHA UWAJIBIKAJI WA KAMPUNI

 


*************

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imewataka Wakurugenzi na Wamiliki wa Makampuni kuendelea kuwasilisha taarifa za Wamiliki Manufaa kwa wakati ili kuwa na uwazi na uwajibikaji katika kampuni husika.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Sehemu ya Makampuni wa BRELA Bi. Leticia Zavu, katika warsha maalum ya uhamasishaji wadau kuhusu Kanuni za Wamiliki Manufaa, inayofanyika tarehe 08-09 Juni, 2022, katika ukumbi wa Mkapa Soko Matola, Jijini Mbeya.

Bi. Zavu amesema kuwa ushiriki wa wadau katika warsha hiyo unatoa mwanga katika kuelekea mapinduzi ya uwekezaji nchini, huku akisisitiza kuwa uwajibikaji unaenda sambamba na uwazi katika utekelezaji wa majukumu, jambo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“Wadau mnapaswa kutoa elimu hii kwa jamii inayowazunguka, kwani taarifa hizi zinalenga katika kumfahamu mmiliki halisi na chanzo cha fedha za kampuni husika, kwa usalama wa nchi na kupunguza mianya ya ubadhilifu miongoni mwa kampuni, hivyo mkawe chachu katika kufanikisha uwasilishaji wa taarifa hizi ndani ya muda uliopangwa,” amesisitiza Bi. Zavu.

Hata hivyo Bi. Zavu amefafanua kuwa taarifa hizi ni za siri na wanaozichakata wanazifanyia kazi kwa umakini hivyo wadau wasiogope kuwasilisha taarifa hizo.

Aidha ameongeza kuwa Mmiliki Manufaa anayepaswa kuwasilisha taarifa zake BRELA ni yule anayemiliki kuanzia asilimia 5 na zaidi ya uwekezaji kwenye kampuni au kushiriki kufanya maamuzi kwenye kampuni moja kwa moja na taarifa zao zinatakiwa kuwasilishwa kupitia mfumo wa kupokea taarifa za Wamiliki Manufaa unaopatikana kwenye tovuti ya BRELA.

Kwa upande wake Afisa Biashara kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw.Stanley Godwin, amefurahishwa na mwitikio mkubwa wa wadau walioshiriki warsha hiyo na kuahidi kuwa ofisi ya mkoa itaendelea kutoa msaada kwa wadau wanaohitaji huduma za BRELA wakati wote

Post a Comment

Previous Post Next Post