Michezo na Sanaa kuwanufaisha wananchi- Mhe, Mchengerwa


Na John Mapepele 

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Wizara yake ina mikakati kabambe ya kuendeleza sekta za michezo, utamaduni na sanaa ili  kuleta mapinduzi makubwa  yatakayowanufaisha wananchi katika kipindi kifupi ikiwa ni pamoja na kuboresha  tuzo za muziki na filamu   kwa wasanii.

Akizunguza usiku wa kuamkia leo kwenye tamasha la The Dream Concert la Msanii nguli wa Hip Hop nchini Joseph Mbilinyi au jina maarufu la Mr. Two Proud au Sugu ya kutimiza miaka 30 kwenye tasnia na kuzindua kitabu chake kiitwacho “Muziki na Maisha” ambapo amesema Wizara yake inatarajia kufanya mambo makubwa ambayo mbali na kuitangaza Tanzania katika anga za kimataifa yatasaidia kuinua kipato cha wasanii na wanamichezo na kuinua uchumi wa nchi yetu.

Amesema Wizara  pia ina mipango mingi na imekusudia kufanya mambo mengi makubwa  kwa maslahi ya tasnia ya sanaa nchini ikiwemo kuandaa mkutano mkubwa wa wadau wa muziki wa Afrika utakaofanyika  mjini Dar es Salaam Novemba mwaka  huu.

Amesema kupitia mkutano huo kutakuwa na manufaa mengi kwa sekta hiyo ikiwa ni pamoja na  ajira 247 za moja kwa moja kwa watanzania wakati wa maandalizi na uendeshaji wa mkutano huo, kupata pia mafunzo mbalimbali katika masuala ya hakimiliki na hakishiriki, namna ya kusimamia tasnia ya muziki, uzajilishaji na kuutangaza muziki wa Tanzania kimataifa .

Aidha, amesema Wizara ina mkakati wa kumaliza changamoto ya viwanja vya michezo na vya ndani   vitakavyojengwa Dar es Salaam na Dodoma ambapo hadi sasa wadau wamejitokeza kwa ajili ya ujenzi wa viwanja hivyo.

Pia amesema kwa kushirikiana na wadau tayari Wizara imeshaanza kuandaa tuzo kubwa za Muziki Barani Afrika za MTv kwa mwaka 2023 na kusisitiza kuwa tuzo hizo ni miongoni mwa tuzo zinazovutia watu wengi duniani ambapo amefafanua kwamba watu mashuhuri zaidi ya elfu kumi hushiriki  na kwamba  yanaangaliwa na zaidi ya watu bilioni moja na nusu.

Amemshukuru Mhe. Rais kwa kutenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwenye Mfuko wa Sanaa kwa ajili ya wasanii ambapo amesema fedha hizo zitasimamiwa  kikamilifu.

Katika hafla hiyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Utamadunio, Sanaa na Michezo kukamilisha mchakato wa “blank tape” ambao  ni chanzo  kingine cha kukusanya mirahaba kwa ajili  ya Wasanii na Wabunifu.

Post a Comment

Previous Post Next Post