BRELA YAIBUKA MSHINDI WA PILI KATIKA MAONESHO MOROGORO




                                    **************

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeibuka mshindi wa pili kati ya taasisi 15 za Serikali zilizoshiriki kutoa huduma kwenye maonesho ya Tano ya Mifuko ya Programu za Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, mkoani Morogoro.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo ya ushindi wa pili na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), jana tarehe 14 Mei, 2022, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amesema, ushindi huo umetokana na huduma ambazo maafisa wa BRELA wamekuwa wakizitoa kwa wananchi wa Manispaa ya Morogoro wakati wote wa maonesho.

Bw. Nyaisa amesema wakati wote wa maonesho wananchi wamefurika kwa wingi katika banda la BRELA kupata elimu na kurasimisha biashara zao huku wengi wakikamilisha usajili wa majina ya biashara na kutoka na cheti cha usajili papo kwa papo.

“Lengo kuu la kushiriki Maonesho haya ni kutoa huduma bora na kwa muda mfupi, ili kufanikisha hilo wafanyakazi wote wamekuja na vitendea kazi, hivyo mwananchi akifika banda la BRELA anapata majibu ya maswali yake yote pamoja, ushauri na huduma ya papo kwa papo,” amefafanua Bw. Nyaisa.

Bw. Nyaisa amewasihi wafanyabiashara kutumia mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao kurasimisha biashara zao kwani huduma hiyo kwa sasa ni rahisi na inamuwezesha muombaji kupata huduma bila kufika katika ofisi za taasisi hiyo.

Aidha Bw. Nyaisa amesema kuwa mfumo uliopo sasa wa urasimishaji biashara ni rahisi na rafiki zaidi kwa waombaji wote walio mjini na vijijini, hivyo ni vyema wafanyabiashara kuacha tabia ya kuwatumia “vishoka” kurasimisha biashara zao.

“Kwa sasa mfanyabiashara sio lazima kufika kwenye ofisi za zetu, unaweza kupata huduma ukiwa hata sebuleni kwako na ukapata cheti bila ya usumbufu wowote,”amesisitiza Bw. Nyaisa.

Taasisi iliyoshinda nafasi ya kwanza katika maonesho hayo yaliyohitimishwa jana ni Shirika la Posta Tanzania, huku Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ikichukua nafasi ya tatu.

Post a Comment

Previous Post Next Post