UEFA LIVE DAR-MHE. MCHENGERWA

Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema kilele cha mashindano ya 67 ya UEFA baina ya Timu ya Real Madrid na Liverpool yataoneshwa mubashara nchini kwenye daraja jipya la Tanzanite jijini Dar es Salaam kupitia DStv  ambapo vivutio mbalimbali vya utalii vitaonyeshwa  moja kwa moja  hivyo kutoa fursa kwa mamilioni ya wapenzi wa soka kutoka nchi zote za Afrika na dunia kushuhudia shindano hilo na vivutio vya utalii kutoka Tanzania.

Akizungumza kwenye kipindi cha Powerbreakfast kinachorushwa na kituo cha Redio cha Clouds Fm leo Mei 17, 2022 jijini Dar es Salaam. Mhe, Mchengerwa amesema mbali na  kurusha mubashara  mechi hiyo yenye mvuto mkubwa  hapa nchini na duniani kote pia Filamu ya Royal Tour itaonyeshwa  kabla  ya kuanza  kwa mechi hiyo ambapo ametoa wito kwa  wananchi kujitokeza  kushuhudia  tukio hilo la kihistoria.

Amefafanua kuwa wakati wa Filamu hiyo ya kihistoria iliyomshirikisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan ambayo imefungua Tanzania duniani, kutachezwa droo ambapo washindi watatu watakaopatikana watatembelea  vivutio mbalimbali vya utalii nchini kwa ufadhili wa Bodi ya Utalii nchini(TTB) na Kampuni ya Heinken.

Aidha, amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendelea  kutumia  sekta za michezo  na Sanaa kuitangaza Tanzania na vivutio  vyake  duniani kwa kuwa zimebeba idadi kubwa ya Tanzania  na kuongeza kuwa  sekta hizo ndiyo nguvu shawishi ya Serikali zinazowapa watanzania wengi zaidi furaha  na faraja.

“Nipende kumpongeza Rais wetu kwa kazi kubwa sana na mikakati thabiti anayoifanya hivi sasa ya kuifungua Tanzania kupitia sanaa na michezo ambapo hivi karibuni ameandika historia kwa kushiriki moja kwa moja katika kuandaa filamu ya Royal Tour” ameongeza Mhe. Mchengerwa.

Ametaja baadhi ya mikakati mingine inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Mhe Samia Suluhu Hassan  kuifungua na kuitangaza Tanzania duniani kupitia Sanaa na michezo kuwa  ni pamoja na kuandaa mashindano  makubwa barani Afrika  ya tuzo za wasanii  ili  yafanyike hapa nchini  yanayojulikana  kama MTV Afrika Awards hapo mwakani,  kuandaa mkutano wa marais wa mashirikisho ya soka utakaohudhuriwa na zaidi ya nchi 54 za Afrika  jijini Arusha ambapo Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) anatarajiwa  kuhudhuria pamoja  na kufikiria  kuandaa  mashindano makubwa ya soka  Afrika  kuanza kufanyikia hapa nchini. 

Pia ameongeza kuwa  tayari Serikali kupitia Wizara anayoiongoza inakamilisha  michoro kwa ajili ya kujenga kumbi za kisasa za michezo na  maonesho ya sanaa  ambapo moja  inatarajia kuchukua takribani watu elfu ishirini jijini Dar es Salaam na nyingine yenye uwezo wa kuchukua watu elfu kumi na tano jijini Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Heinken Nchini ambayo ndiyo mdhamini mkuu  wa tukio hilo Bi Fatma Mnaro amefafanua kuwa lengo la kuonesha mubasha  kilele cha UEFA hapa nchini  kupitia DSTv  ni kutaka kuwafanya  wapenzi wa soka walione shindano hilo kwa ubora wa hali ya juu kama ambavyo watakavyoshuhudia wale ambao watahudhuria mtanange huo nchini  Paris nchini Ufaransa.

Aidha,  Bi. Mnaro ameongeza kuwa pamoja na kurushwa mubashara  kwenye Daraja la Tanzanite  pia  kuna sehemu  mbalimbali  za majiji makubwa ambazo pia zitaonesha ambazo ni pamoja na The Cask jijini Mwanza, City Pub jijini Mbeya, Arusha na Capetown Fish Market, Samakisamaki na Triple 777 jijini Dar es Salaam.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post