MHE. MCHENGERWA- TANZANIA YAANZA MAANDALIZI YA KURATIBU AFCON

Na John Mapepele

Serikali ya Tanzania na Qatar imefanya mazungumzo ya kuimarisha mahusiano kwenye sekta za michezo, sanaa na utamaduni ambayo  yanalenga kusaidia Tanzania  kufanya mapinduzi makubwa  kwenye sekta za michezo nchini ikiwa ni pamoja na Tanzania kuratibu mashindano makubwa ya Afrika ya Soka hususan Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON ifikapo mwaka 2027.

Maongezi hayo yamefanywa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa kwa upande wa Serikali ya Tanzania na Balozi wa Qatar nchini, Mhe. Hussain Ahmad Al-Homaid leo Mei 27, 2022 Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa tayari Serikali imeshaomba  miundombinu ya soka inakayotumika kwenye  mashindano ya kombe la Dunia yanayotarajiwa  kufanyika nchini Qatar ambapo Mhe, Balozi Al-Homaid amesema  Serikali yake itazingatia  ombi hilo kwa kuipa kipaombele nchi ya Tanzania.

“Maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na dhamira  ya Serikali kuona kuwa Tanzania inakwenda  kuratibu AFCON 2027” amefafanua Mhe Mchengerwa.

Amesema Serikali imejipanga  kuboresha na kujenga  miundombinu ya kisasa  ikiwa ni pamoja na viwanja vitatu ambayo vitasaidia Tanzania  kufuzu  vigezo  vya kupata nafasi ya kuratibu  mashindano haya.

Ameongeza kuwa katika kuimarisha ushirikiano baina  ya nchi yetu na Qatar,  Wizara inakwenda kuandaa tamasha kubwa la wasaanii  ikiwa ni pamoja na wasanii wa  uchoraji na uchongaji  ambapo  amefafanua kuwa Tanzania ina hazina kubwa  ya wasanii ambao wamekuwa  wakitengeneza  kazi nzuri zinazouzwa kwa  thamani kubwa duniani.Aidha, amesema Tanzania inakwenda kuadhimisha siku ya Kiswahili duniani kuanzia Julai mosi hadi kilele chake Julai saba  ambapo amesema kwenye  maadhimisho ya siku hiyo mambo mbalimbali yatafanyika ikiwa pamoja na maonesho ya muziki wa taarabu na vyakula  vya asili  kutoka  kwenye makabila  ya Tanzania.Baada ya mazungumzo hayo ambayo Mhe. Mchengerwa ameambatana na Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu Saidi Yakubu na Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusufu Singo alipata fursa ya kukagua miundombinu ya Uwanja wa Benjamini Mkapa na  Mashindano ya Afrika ya Riadha ambayo yamekuwa yakiendelea uwanjani  hapo.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post