Na John Mapepele
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu ameipongeza Wizara ya utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kazi kubwa inayofanya ya kuitangaza Tanzania duniani kupitia sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Mhe. Samia ametoa kauli hiyo wakati akipokea Kombe la Dunia la FIFA leo Mei 31, 2022 Ikulu jijini Dares Salaam kutoka kwa kiongozi kikosi cha ziara ya kombe hilo hapa nchini na mchezaji nguli wa Brazil Juliano Belletti.
Amesema Wizara hiyo imekuwa ikifanya ubunifu mkubwa wa kuitangaza Tanzania ambapo katika siku za hivi karibuni kwa kushirikiana na wadau waliandaa tukio la kutazama mbashara fainali za UEFA kupitia DSTv kwenye Daraja jipya la Tanzanite lililopo jijini Dar es Salaam hivyo kuifanya dunia kuendelea kuilifahamu daraja hilo la kisasa na Tanzania kwa ujumla wake.
"Lakini kutumia lile daraja na wakaonyesha na tukaonekana ulimwengu mzima ile ni jitihada kubwa, na wameonesha kwamba Tanzania tuna vivutio vinavyoweza kutumika na ni ubunifu mkubwa” amesisitiza Mhe. Rais Samia.
Pia, Mhe. Rais amepongeza kwa kuendelea kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ya mpira wa miguu na kufafanua kuwa yameendelea kuitangaza Tanzania duniani.
Aidha, alitaka ujio wa kombe la dunia utumike ari kubwa zaidi kwa timu za taifa za wanawake kuendelea kufanya vizuri zaidi ili ziweze kufika kwenye mashindano ya dunia hatimaye kuitangaza Tanzania na vivutio vyake.
Kuhusu kuratibu mkutano mkuu wa mashindano ya soka ya Kombe la shirikisho la Bara la Afrika (CAF) Mhe. Rais na amesisistiza kutumia vizuri nafasi hizi kutangaza vivutio mbalimbali vya Tanzania na hatimaye kuinua uchumi wa nchi yetu.
Akimkaribisha kutoa hotuba, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Mohamed Mchengerwa amemshukuru Mhe. Rais kwa kuunda wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuendelea kumwamini na kumteua kuongoza Wizara hiyo muhimu ambayo ni nguvu shawishi ya nchi ambapo amesisitiza kuwa wizara yake itaendelea kuwa bunifu zaidi.
Amesema kupitia michezo Tanzania imepata heshima kubwa ambapo amesema kwa sasa Serikali inatekeleza programu ya kuibua vipaji wanamichezo na wasanii ya mtaa kwa mtaa, ujenzi wa shule za michezo,kujenga viwanja vya kisasa vya ndani kwenye miji ya Dar es salaam na Dodoma na sasa kuhakikisha timu za taifa ili ziweze kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa ikiwa ni pamoja na timu ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17 ya Serengeti Girls ili ifuzu kuingia kombe la dunia.
Amesema kinachopaswa kufanya sasa ili kuleta mapinduzi kwenye michezo ni kila mtu kutekeleza wajibu wake huku akinukuu kauli ya baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyoitoa mwaka 1978 ambayo alisema” Inawezekana endapo kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake”