Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Mohamed Mchengerwa amemwakilisha, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa kwenye ufunguzi wa maabara ya kisasa ya Komputa iliyojengwa kwa ufadhili wa klabu ya Baseball Dodgers ya Marekani kupitia Chama cha Mchezo wa Baseball/Softball Tanzania.
Tukio hilo amelifanya leo, Aprili 19, 2022 kwenye Shule ya Sekondari ya Azania jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa taasisi za michezo wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Saidi Yakubu na wadau mbalimbali.
Mhe. Mchengerwa ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa michezo kujitokeza kuwekeza katika miundombinu ili sekta ya michezo iweze kusonga mbele
Ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuendelea kukuza sekta ya Michezo na Sanaa kwa kushikiana na wadau wenye utashi wa kuwekeza katika sekta hizo.
"Mpango wa Serikali ni kufanya michezo iwe biashara".ameongeza Mhe, Mchengerwa
Aidha, amesema tayari Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na wanamichezo ili kuhakikisha lengo la kuboresha michezo hatimaye kutoa ajira na kuongeza uchumi liweze kufikiwa.
"Nyote mnakumbuka , hivi karibuni Serikali imepitisha Sheria ya uundaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ambapo kiasi cha asilimia 5 ya fedha zinazitokana na kodi ya michezo zitaingizwa katika huu ili kuendeleza sekta ya michezo nchini". Amesisita Mhe. Mchengerwa
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto ya miundombinu ya michezo ambapo kwa sasa tayari imetenga shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya kupumzikia kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Geita.
Pia amesema Wizara yake inakwenda kuratibu kombe la Samia CUP mtaa kwa mtaa na kusisitiza kuwa mashindano hayo yana lengo la kusaka vipaji vya wachezaji kuanzia ngazi ya chini ya mtaa na kijiji.
Katika hatua nyingine Mhe. Mchengerwa amesema Serikali ya Rais Samia kupitia Wizara yake imechangua Shule ya Azania na Kibasila katika mkoa wa Dar es Samaam ili zijengewe miundombinu ya michezo katika program ya kujenga shule mbili za michezo kila mkoa.
"Hivi ninavyosema tayari tumetengewa bilioni mbili kwa ajili ya kazi hiyo na ninaagiza hapa Azania iwe shule ya kwanza kujengewa miundombinu hiyo" amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Mhe. Mchengerwa pia amepata fursa kuangalia timu ya taifa ya baseball ikifanya mazoezi katika uwanja wa shule ya Azania