BARABARA YA SONGWE,VWAWA KUKAMILIKA JUNI, 2022

 NAIBU Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amesema Serikali inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Mahenje - Ndolezi - Hasamba hadi Vwawa ambayo ni muhimu kwa utalii na usafirishaji wa mazao mkoani Songwe.


Akijibu swali Bungeni leo lililoulizwa na Mbunge wa Vwawa Mhe. Japhet Hasunga, lililotaka kujua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, Naibu Waziri Kasekenya amelihakikishia Bunge kwamba ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kilometa 4.5 utakamilika ifikapo mwezi Juni, mwaka huu.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Igawa – Mbeya – Tunduma ili kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo muhimu kiuchumi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya ameliambia Bunge kuwa jukumu la usafi wa barabara na mifereji ikiwa ni pamoja na kuzibua makalvati ni la msimamizi wa barabara husika, hivyo kwa barabara Kuu na za Mikoa zinasimamiwa na TANROADS na barabara za Mijini na Vijijini zinasimamiwa na TARURA.

Eng. Kasekenya alikuwa akijibu swali la Mhe. Naghejwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge Viti Maalum aliyetaka kujua ni nani hasa anayehusika na usafi wa mitaro pembeni mwa barabara.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akijibu swali katika mkutano wa saba wa Bunge unaoendelea, jijini Dodoma.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Post a Comment

Previous Post Next Post