Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa leo Aprili 24, 2022 amezungumza na wachezaji wa Timu ya Simba masaa machache kabla ya kuingia kwenye mechi ya marudiano na Orlando Pirates katika mashindano ya kombe la Shirikisho barani Afrika na kuwatakia kila la heri katika mchezo huo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Mchengerwa ameongea na wachezaji wa Simba kupitia simu ya Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ambapo ametaka wachezaji kucheza kwa moyo huku wakitambua kuwa ushindi wa Simba leo utaiweka Tanzania katika ramani ya Afrika ya nchi zenye vilabu vinavyofanya vizuri.
Aidha, ameongeza kuwa watanzania na Serikali ipo bega kwa bega na timu hiyo na kwamba wazingatie zaidi mchezo na wapuuze baadhi ya maneno kuhusu mambo ya usalama kwakuwa watanzania na waafrika kusini ni ndugu na marafiki na mchezo siyo uadui.
" Mheshimiwa Rais anamatarajio makubwa sana na mchezo wa leo kwani ni dhamira yake kiuona nchi yetu inafanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa" amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amesema kwa sasa akili na masikio ya watanzania yapo nchini Afrika Kusini na amewataka wachezaji na watanzania wote kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele katika mchezo wa leo ili tuweze kushinda.
Timu ya Simba inatarajia kushuka dimbani kucheza na Orlando Pirates ya Afrika ya Kusini majira ya saa moja usiku kwa saa za Tanzania.
Katika mchezo wa kwanza wa robo fainali Simba iliishinda Orlando 1-0 katika uwanja wa Benjamini Mkapa Aprili 17, 2022 kwa mkwaju wa penati.