Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameipongeza timu ya Simba kwa kufuzu kuingia robo fainali ya ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika baada ya kuibamiza vibaya timu ya US Gendarmerie 4-0 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo.
Mhe. Mchengerwa ametoa pongezi hizo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mpambano huo ambapo amesema ushindi huo ni ushindi wa kihistoria.
"Ninaipongeza Timu ya Simba kwa ushindi wa kishindo kuelekea kwenye Robo Fainali ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika. Kama Taifa, tunajivunia kwa ushindi huo mnono unaoitangaza Nchi yetu kimataifa." Amefafanua Mhe. Mchengerwa
Ameitaka Timu ya Simba kufanya maandalizi ya kutosha ili kuweza kufanya vizuri zaidi katika mashindano hayo hatimaye kuchukua kombe na kuendelea kuitangaza Tanzania duniani.
Simba kwenye michuano ya robo fainali inaweza kukutana na TP Mazembe(DR Congo), Orlando Pirates ( Afrika Kusini) na Al Ahly Tripoli (Libya).
Ukiachilia timu hizi nne(4) timu nyingine nne(4) ambazo zimefuzu kuingia robo fainali ya mashindano haya ni pamoja na RS Berkane (Morocco), Pyramids (Misri), Al-Ittihad (Libya) na Al Masry Misri.
Simba inatarajiwa kuanzia nyumbani Uwanja wa Mkapa.