Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameipongeza timu ya Simba kwa ushindi wa goli 1-0 dhidi timu ya Orlando Pirates Aprili 17, 2022 kwenye dimba la Mkapa jijini Dar es Salaam.
Pongezi hizi ameendelea kuzitoa leo baada ya zile alizotoa jana mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo.
Ikumbukwe kuwa Mhe. Mchengerwa jana aliwaongoza maelfu ya watanzania kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan kuishangilia Simba katika uwanja wa Mkapa hatimaye ikatwaa ubingwa huo.
Asubuhi kabla ya mechi hiyo, Mhe. Mchengerwa baada ya kumaliza kushiriki mashindano makubwa ya Qur'an barani Afrika yaliyofanyika kwenye uwanja huo huo wa Mkapa, akiambatana na Naibu Katibu Mkuu wake Said Yakubu alitoa wito kwa watanzania kujitokeza kuja kuishangilia Simba katika mechi hiyo iliyochezwa kuanzia saa moja usiku ili ishinde.
Ubingwa wa Simba ulipatikana kupitia kwa beki kisiki Shomari Kapombe ambaye alipiga penati nzuri ambayo ikazama moja kwa moja wavuni ikimwacha kipa akihangaika kulia na mpira ukimpita kushoto.
Penati hiyo ilitokana na kufanyiwa madhambi mchezaji machachari wa Simba Bernard Morrison.
Mhe. Mchengerwa amesema Simba imeendelea kuutendea haki uwanja wake wa nyumbani kwani imekuwa ikifanya vizuri kwenye michezo mingi akiwa nyumbani.
Simba Sc itawafuata Orlando Pirates Fc katika mechi ya marudiano ambayo itapigwa Johannsburg nchini Afrika Kusini, mechi itakayopigwa Aprili 24.
Ameitaka iendelee kufanya mazoezi ya kutosha ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuvuka katika hatua inayofuata.
Wakati huo huo, Mhe. Mchengerwa ameipongeza timu ya Taifa ya wanawake U17 ya Serengeti Girls kwa kuendelea kushinda mechi za kufuzu mashindano ya kombe la dunia baada ya kuibamiza Burundi bao nne kwa nunge huku akisisitiza kuendelea kujioa zaidi kwa mchezo ujao.
"Nimefurahishwa sana na Serengeti kwa kuendelea kutuheshimisha, Serikali ipo bega kwa bega na nyie katika kila hatua ili tuchukue kombe hili" amefafanua Mchengerwa
Pia Waziri Mchengerwa ameipongeza timu ya Taifa ya kuogelea kwa kuibuka na medali 13 kwenye mashindano ya Kanda ya Nne ya Afrika yaliyofanyika Lusaka nchini Zambia na kumalizika jana Aprili 17, 2022.