Mwenyekiti wa Mfuko wa Hisani wa Kujitolea, Kuongoza na Kubadilisha Beatus Rwechungura akimkabidhi risiti ya malipo ya Tshs.2,655,000/= Edna Michael leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya gharama za upasuaji wa moyo wa mtoto wake anayesubiri kufanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwaeleza wadau kutoka Mfuko wa Hisani wa Kujitolea, Kuongoza na Kubadilisha kuhusu magonjwa ya moyo kwa watoto walipotembelea Taasisi hiyo leo kwa ajili ya kukabidhi risiti za malipo ya Tshs.8,750,000/= ikiwa ni gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto watatu. Kulia ni Ramadhani Iddi ambaye mtoto wake amelipiwa Tshs.2,895,000/= kwa ajili ya upasuaji wa moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na wadau kutoka Mfuko wa Hisani wa Kujitolea, Kuongoza na Kubadilisha waliofika katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kukabidhi risiti za malipo ya Tshs.8,750,000/= ikiwa ni gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto watatu
**********************************************
Wananchi wanaohitaji kulipia gharama za matibabu ya wagonjwa wa moyo wameshauriwa kufika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuwatambua wagonjwa ambao hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu pia kufahamu gharama halisi za matibabu yao.
Ushauri huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na wadau kutoka Mfuko wa Hisani wa Kujitolea, Kuongoza na Kubadilisha waliofika JKCI kwa ajili ya kukabidhi risiti za malipo ya gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto watatu.
Prof. Janabi alisema wananchi wanaotaka kulipia gharama za matibabu ya wagonjwa wa moyo wafike katika Taasisi hiyo au wapige simu, wataoneshwa njia sahihi ya kufanya malipo ikiwa ni pamoja kupewa gharama halisi ya matibabu na kuoneshwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa matibabu.
“Siku hizi tumekuwa tukiona katika mitandao ya kijamii watu mbalimbali wakichangisha fedha za matibabu ya wagonjwa. Kwa upande wa wagonjwa wa moyo ninawaomba wananchi wanaotaka kusaidia wagonjwa wafike katika Taasisi yetu , wataoneshwa wagonjwa husika na kupewa taratibu za kufanya malipo hii itawasaidia kuepuka kutapeliwa”,.
“Ninawashukuru sana ndugu zetu hawa leo hii wamelipa Tshs.8,750,000/= kwa ajili ya gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto watatu ambao walezi wao hawana uwezo wa kulipia matibabu yao. Tumewaonesha watoto hao kabla ya kufanyiwa upasuaji na watakuja tena kuwaona baada ya kufanyiwa upasuaji. Wamechukuwa namba za simu za walezi wao ambao watawasiliana nao ili kujua maendeleo ya watoto”, alisema Prof. Janabi.
Mkurugenzi huyo Mtendaji ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo aliisistiza jamii kuwa na tabia ya kuchangia gharama za matibabu kwa wagonjwa ambao hawana uwezo kwani Serikali peke yake haiwezi kwa kuwa gharama za matibabu ni kubwa kuna vifaa ambavyo vinatakiwa kununuliwa na vinapatikana nje ya nchi.
Kwa upande wake Beatus Rwechungura ambaye ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Hisani wa Kujitolea, Kuongoza na Kubadilisha alisema kikundi chao kina watu sita ambao ni marafiki wa siku nyingi huwa wanatoa michango ya mara kwa mara kwa ajili ya kusaidia jamii inayowazunguka.
“Tulichangishana tukapata kiasi cha Tshs.8,750,000/= fedha ambazo tumelipia gharama za matibabu ya upasuaji wa moyo kwa watoto watatu na tuliamua kusaidia watoto kwasababu wanauhitaji na tunatengeneza maisha yao ya baadaye”, alisema Rwechungura.
Rwechungura alisema wamefika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na kutembelea wodini wameona kuna uhitaji mkubwa, waliomba watu wenye uwezo wa kuchangia wasaidie chochote watakachoweza kitasaidia na kuwa na matokeo mazuri katika maisha ya watoto.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Asha Salum alishukuru kwa wageni waliowapata ambao wamewasaidia watoto wenye matatizo mbalimbali kwa kuwalipia gharama za matibabu ya moyo.
Asha alisema uhitaji ni mkubwa kuna watoto wanaofika kutibiwa katika Taasisi hiyo na hawana bima za afya na kuna ambao wanabima lakini gharama za matibabu ni kubwa na wazazi hawana uwezo wa kulipia. Hivyo basi wanalazimika kuomba msaada kwa wadau mbalibali ikiwa ni pamoja na Taasisi kulipia gharama hizo.
“Watoto hawa pia wanamahitaji mengine ya muhimu kama vile diapers, sabuni, dawa za meno, miswaki na vitu vya kuchezea ninaomba watu mbalimbali ambao wataguswa waweze kuwasaidia”, alisisitiza Asha.
Nao wazazi ambao watoto wao wamelipiwa gharama za matibabu walishukuru kwa moyo wa upendo ulioonesha na wasamaria wema hao na kuwaomba wananchi wengine waweze kuwasaidia watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo ambao wazazi wao hawana uwezo wa kulipia gharama hizo.