Na. John Mapepele.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa leo Aprili 5,2022 jijini Dodoma amezindua Mkakati wa Maendeleo ya Michezo wakati alipofungua rasmi Kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo huku akipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mafanikio lukuki yaliyopatikana katika kipindi hiki kutokana na mikakati madhubuti iliyojiwekea.
Amesema kuwa Wizara ya utamaduni, sanaa na Michezo inafanya kazi kubwa ambayo imekuwa na mchango mkubwa kwa pato la taifa, utulivu wa nchi na mshikamano miongoni mwa watanzania.
"Kazi kubwa mnayoifanya inaleta furaha ndani ya mioyo yetu. Sifa ya nchi yetu ambayo ipo ndani na nje imetokana na umoja, utulivu na amani na mshikamano tulionao” amefafanua Mhe. Majaliwa
Mhe. Majaliwa amesema sekta ya Sanaa imeweza kuitangaza Tanzania na kwamba nchi yetu imepata heshima kubwa katika michezo kutokana na michezo mbalimbali kufanya vizuri huku akitolea mfano wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Walemavu Tembo Warriors ambayo imefuzu kuingia katika michuano ya kombe la dunia la mchezo huo.
“Hadi ninapozungumza sasa tayari wachezaji wanne (4) wa Timu yetu ya Tembo Warriors wamesajiliwa kwenye timu za kimataifa katika mataifa ya nje ukiachilia mbali michezo mingine kama ngumi, kuogelea ambayo pia inafanya vizuri sana” ameeleza Mhe. Majaliwa.
Ameongeza kuwa Tanzania imepiga hatua kufika uchumi wa kati ambapo amesema sekta ya sanaa inamchango mkubwa katika hilo ambapo amesisitiza kuwa huwezi kutenganisha utamaduni na maendeleo yaliyofikiwa hivi sasa hapa nchini.
Ametumia kikao hicho kutoa maelekezo mbalimbali ya Serikali kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara nyingine kwenye eneo la Utamaduni na Michezo ili kuleta maendeleo katika sekta hizo.
Akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu kutoa hotuba yake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Mchengerwa amewashukuru viongozi wakuu wa nchi kwa kutoa kipaumbele kwenye sekta anazoziongoza huku akisema sekta za michezo na sanaa zina mchango mkubwa kwa taifa.
Amesema sekta hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha ajira rasmi na zisizo rasmi, zinachangia katika kuimarisha afya za wananchi kupitia mazoezi hivyo kupunguza magonjwa yasiyoambukiza, kukuza utalii na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.
Aidha, amesema lengo la vikao hivyo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao maafisa michezo na utamaduni limeendelea kutimia na amefafanua kwamba vimeleta matokeo chanya ambapo ametolea mfano wa kurasimishwa kwa tasnia ya Sanaa na lugha ya Kiswahili kupata msukumo mkubwa katika kipindi hiki.
Kikao hicho kimepambwa na birudani za kikundi cha wasanii kutoka Dodoma ambacho kilimkosha Mhe. Waziri Mkuu na kumfanya awaongoze maafisa Michezo na Utamaduni kuanza kucheza na kukituza.