TBA YAENDELEA NA KASI YA UJENZI WA NYUMBA 150 JIJINI DODOMA

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) unaendelea na ujenzi wa nyumba 150 za makazi ya watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma kwa lengo la kupunguza uhaba wa nyumba kwa watumishi hao mkoani Dodoma.

Mradi huo ambao utakuwa na nyumba 3500 unajengwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza kwa sasa zinajengwa nyumba 150 ambazo hadi kufika mwezi wa tano mwaka huu zinatarajiwa kukamilika na kuanza kuwapangisha watumishi wa serikali kwa bei nafuu kwa lengo la kuwasaidia kujikimu kimaisha.

Kumekuwa na changamoto kubwa ya uhaba wa nyumba kwa watumishi wa Serikali  wanaohamia mkoani Dodoma kutokana na idadi yao kuwa ni kubwa ukilinganisha na nyumba zilizopo, lakini TBA imeendelea kujitahidi kutatua changamoto hiyo kwa kubuni na kujenga nyumba zingine mpya ukiwemo mradi huu mkubwa wa nyumba zinazoendelea kujengwa katika eneo la Nzuguni. 

Aidha, nyumba ambazo TBA inazisimamia na kupangisha watumishi wa Serikali bei zake  ni kati ya shilingi 150,000 hadi 450,000 kulingana na aina ya nyumba pamoja na ukubwa wa eneo husika.  Pia mtumishi anaweza kulipa kodi hiyo kwa awamu mbalimbali au kama ataweza analipa yote kwa pamoja.




Post a Comment

Previous Post Next Post