TFRA YATOA ELIMU MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA

 Na Mwandishi Wetu, Lindi

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Mikoa ya Lindi na Mtwara imetoa elimu kwa vitendo  kupitia  mashamba darasa  kwa ajili ya kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwa lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya mahindi na mpunga.

Katika jitihada zake za kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kwenye  mikoa  hiyo serikali kupitia TFRA imeanzisha mashamba darasa katika halmashauri za Ruangwa, Mtama, Mtwara na Masasi ambapo wakulima kupitia vikundi  vyao wamepata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa njia ya vitendo.

Akitoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea katika halmashauri hizo, Afisa Udhibiti Ubora kutoka TFRA Aziz Mtambo amesema  mkulima hawezi kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao shambani pasipo kutumia mbolea.

Mtambo amesema   ili  mmea ukue na kutoa mavuno bora shambani unahitaji virutubisho vya kutosha  na virutubisho hivyo hupatikana kwenye udongo wenye rutuba  ya kutosha.

Ameongeza kuwa upungufu wa virutubisho unapotokea shambani huhitajika kuongezwa kwa kuweka mbolea ambayo  amesema huwa na virutubisho mbalimbali ikiwemo naitrojeni, fosiforasi na potasiamu.

Mtaalamu huyo amesema kuwa mambo muhimu anayotakiwa kuzingatia mkulima kabla  ya kuweka mbolea ni pamoja na afya ya udongo wa shamba, aina ya mbolea itakayotumika na upatikanaji wa mbolea husika.

Amesema matumizi sahihi ya  mbolea ni lazima yazingatie kanuni  bora zingine  za kilimo ikiwemo kuandaa shamba kwa wakati, matumizi ya mbegu bora, kupalilia, kupiga madawa ya kuzuia na kuua wadudu na magonjwa mbalimbali na kuvuna kwa wakati unaostahili.

“Ni vema wakulima mkafahamu kuwa  matumizi sahihi  ya mbolea ni pamoja na kutumia mbolea sahihi, kiwango sahihi , wakati sahihi na sehemu sahihi ili kuleta matokeo  mazuri yatakayoongeza tija katika uzalishaji  wa mazao”,   alisema Mtambo.

Naye Afisa Kilimo wa Kata ya Kitere iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya  Mtwara   Swalehe Tendwa amesema kupima afya ya udongo inasaidia kutambua virutubisho vilivyopo kwenye udongo  na vipo kwa kiasi gani na  uchachu uliopo.

Tendwa ameongeza kuwa faida za kupima afya ya udongo ni pamoja  na kupunguza gharama za uzalishaji kwani mkulima atanunua mbolea kulinganana upungufu uliopo kwenye udongo  wa shamba lake na kutambua kiwango sahihi cha mbolea kinachohitajika.

Aidha amesema uhamasishaji wa matumizi ya mbolea unaofanywa na TFRA kwa kushirikiana na mikoa ya Lindi na Mtwara umeleta mwamko mkubwa kwa wakulima katika msimu huu wa kilimo ambapo wananchi wengi wamekuwa wakipita katika mashamba darasa  hayo ili kujifunza faida za kutumia mbolea katika uzalishaji wa mpunga na mahindi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Lindi Shaibu  Ndemanga  akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashamba darasa hayo  hivi karibuni alisema kuanzishwa kwa mashamba hayo kutaleta hamasa kubwa kwa wakulima wa mikoa hiyo kutaka kutumia mbolea katika uzalishaji wa mazao mbalimbali na hivyo kuongeza kipato.

Amesema mikoa ya  Lindi na Mtwara ina zaidi ya hekta 6,400, 000 zinazofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali,  hata hivyo tija ya uzalishaji kwenye mazao mengi bado ni ndogo.

“Takwimu hizi zinaonyesha uwepo wa utajiri wa maeneo ya kutosha yanayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali lakini bado hatujaweza kutumia fursa hii kwa ukamilifu na moja ya sababu ni kwamba wakulima wengi hawazingatii kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi ya mbolea,” alisema Ndemanga.

Mkuu wa wilaya huyo  amesema mikoa ya Lindi na Mtwara kwa miaka iliyopita imekuwa ikikabiliwa na upungufu wa chakula,  hivyo kusababisha serikali kuleta chakula cha msaada ili kupunguza kutokea kwa baa la njaa.

Mwenyekiti wankikundi cha wakulima cha Tupendane katika halmashauri ya wilaya ya Mtwara Bi. Mary Mapunda ameishukuru serikali  kupitia TFRA kwa kuwaelimisha  kwa vitendo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea kwa kutumia mashamba darasa.

Bi. Mapunda amesema vikundi vya wakulima vimehamasika kushiriki katika hatua zote za mafunzo hayo kwa  vitendo  kwani  elimu hiyo inawasaidia kuelewa kwa haraka kuhusu matumizi sahihi ya mbolea katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.  

Wakulima zaidi ya 60 katika halmashauri za Ruangwa, Mtama, Masasi na Mtwara wanashiriki katika hatua zote zinazofanyika kwenye mashamba darasa hayo  yenye lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea katika uzalishaji wa mazao  ya mahindi na mpunga

Caption.Afisa Udhibiti ubora Aziz Mtambo akitoa mafunzo kuhusu  matumizi sahihi ya mbolea kwa kikundi cha wakulima Kitere katika halmashauri  ya wilaya ya Mtwara
Wakulima wa Kata ya Kitele katika Halmashauri ya wilaya ya Mtwara wakipalilia Shamba darasa kwa ajili ya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya Mbolea.

Kikundi cha wakulima wa  kijiji  cha Chimbila B katika halmashauri ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi wakifanya palizi katika  Shamba darasa kwa ajili ya uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea


1 Comments

Previous Post Next Post