KAZAKHSTAN: SOKO JIPYA LA UTALII TANZANIA

 Na Catherine Mbena TANAPA/ARUSHA


Jumla ya watalii 16 wamewasili leo kutoka nchini Kazakhstan kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro na kupokelewa na uongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) , Ofisi ya Uwakilishi wa heshima wa jamii ya Wakazakhstan Tanzania na kampuni ya Alteza ambao ndio wenyeji wao.

Akizungumza baada ya kuwapokea watalii hao, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Angela Nyaki kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA amesema hili ni soko jipya kwenye sekta ya Utalii na TANAPA italitilia mkazo kuhakikisha kwamba wanapata huduma nzuri ili wawe mabalozi wazuri wa utalii wa Tanzania.

“Tumekuja kuwapokea wageni kutoka Kazakhstan, wamefurahi kuwepo Tanzania na wanatarajia kupanda Mlima Kilimanjaro, watakwenda Hifadhi ya Taifa Serengeti na baadae Tarangire. Naamini kwa mapokezi waliyoyapata watakuwa mabalozi wa utalii wa nchi yetu.” Alisema Kamishna Nyaki.

Kwa upande wake mshauri kutoka uwakilishi wa heshima wa jamii ya wakazakhstan Bw. George Lengeju amesema ofisi ya uwakilishi wa heshima inaangalia uwezekano wa kuanzisha safari kwa ndege za kukodi kutoka Kazakhstan kuja Tanzania na idadi ya watalii kutoka nchi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

Pia Bw. Lengeju amewataka vijana wa kitanzania kuchangamkia fursa ya kujifunza lugha ya kigeni hususani lugha ya kirusi ili kurahisisha mawasiliano baina ya wenyeji na wageni hawa kutoka Kazakhstan. Pia amewatoa shaka wageni kutoka Khazakhstan kwakuwa nchini Tanzania kuna jumuiya kubwa ya watu wanaozungumza lugha ya kirusi na pia lugha hii hufundishwa katika Chuo kikuu cha Dodoma na kupelekea kutokuwepo kwa Changamoto ya mawasiliano.

Jumla ya watalii 40 kutoka nchini Kazakhstan wamekuja Tanzania katika wiki hii ambapo wamekuja katika makundi matatu tofauti na leo wamewasili wengi zaidi ambapo watapanda mlima Kilimanjaro, watembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti na Tarangire.

Hii ni matokeo ya juhudi zinazofanya na TANAPA na wadau wengine kuhakikisha si tu kwamba watalii kutoka masoko yaliyozoeleka wanatembelea Tanzania lakini pia tunafungua masoko mapya.






Post a Comment

Previous Post Next Post