MOROCCO YAKUBALI KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KWENYE MICHEZO

Na. John Mapepele

Waziri wa utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Februari 15, 2022 amekutana na Balozi wa Morocco nchini Mhe. Zakaria Elgoumiri na kufanya mazungumzo ya kuendeleza sekta za michezo, utamaduni na Sanaa ambapo  Balozi amesisitiza serikali yake ipo tayari kushirikiana na Tanzania kwa faida ya wananchi wa nchi hizo.

Mhe. Mchengerwa amesema Serikali ya Tanzania na Morocco zimekuwa na uhusiano mzuri katika sekta  hizo  toka  muda mrefu  hali ambayo  imewafanya  viongozi wakuu wa nchi zote  kufanya ziara na  kubadilishana  uzoefu  wa sekta hizo.

Akiwa katika kikao hicho ambacho aliambatana na Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa michezo nchini Yusufu Singo na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo (BMT) Neema Msitha wamekubalina  na ujumbe wa Mhe. Balozi wa kuendelea kushirikiana  kwenye sekta  hizo. 

Ameyataja  baadhi ya maeneo ya kipaombele ambayo yanakwenda  kufanyiwa kazi kuwa ni ujenzi na ukarabati wa  miundombinu ya michezo, maeneo ya tamthilia na filamu pamoja na kushirikiana  kwa pamoja  kuandaa  matamasha ya Sanaa na Utamaduni.

Mhe. Mchengerwa amewakaribisha kushiriki katika matamasha  makubwa ya kihitoria ya Serengeti litakalofanyika jijini Dodoma Machi 12,2022 na Tamasha la Kimataifa la Utamaduni na Sanaa Bagamoyo.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Elgoumiri amesema Serikali ya nchi yake inafurahishwa na Sera na diplomasia ya uchumi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivyo ipo tayari kuendelea kushirikiana  na ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.

Ameuomba upande wa Tanzania kukamilisha andiko  iliutiaji Saini  ufanyike mara moja.

“Tupo tayari kusaini andiko la kukuza ushirikiano kwenye  maeneo tuliyokubaliana  wakati wowote andiko litakapokuwa tayari”. Amesisitiza Mhe Elgoumiri

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa na Balozi wa Morocco nchini Tanzania  katika picha ya pamoja leo Februari 15, 2022 jijini Dar baada ya kumaliza  kikao cha kushirikiana  katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.


Post a Comment

Previous Post Next Post