MHE. MCHENGERWA ATOA MAAGIZO MAZITO TaSUBa

 

Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameitaka Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) na wadau mbalimbali wakiwemo wazalishaji wa muziki hapa nchini kutengeneza muziki wa kitanzania ambao utalitambulisha taifa la Tanzania duniani.

Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Februari 9, 2022 alipofanya ziara   ya kikazi kwenye taasisi hiyo mjini Bagamoyo akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wake Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu. Saidi Yakubu.

Amesema kutokana na ukongwe wa chuo hicho ni muhimu kikafanya kitu kikubwa ambacho kitasaidia  kuutambulisha  utamaduni wa Tanzania duniani na  kutoa ajira kwa vijana  wengi.

Aidha Mhe, Mchengerwa ameitaka Wizara yake kuanzisha kituo cha Televisheni na Redio kitakachokuwa na studio maalum ambayo itasaidia kuzalisha, kukuza na kunoa wasanii kutoka mitaani na vijijini nchi nzima, pia viongozi wa sanaa na wafanyakazi katika sekta ya utamaduni sambamba na kuzalisha kazi za sanaa pamoja na huduma za medianuai (multimedia).

Mkakati wa kusaka vibaji vya wasanii mtaa kwa mtaa nchi nzima ni jambo aliloliasisi Mhe. Mchengerwa mara baada ya kuteuliwa hivi karibuni kuiongoza Wizara hiyo ambapo sasa anataka kuanzishwa kwa kituo cha televisheni na redio  ambacho kazi yake kitakuwa kikitangaza maudhui ya Utamaduni na Sanaa za kitanzania  pia michezo mbalimbali ili  kuuza  utamaduni wa mtanzania kimataifa.

Aidha, Mhe. Mchengerwa ameelekeza TaSUBa  kuanza mara moja  maandalizi ya Tamasha la kimataifa la Sanaa na Utamaduni la mwaka  huu ili liwe bora zaidi kuliko matamasha yote yaliyotangulia pia kutangaza utamaduni kama  bidhaa  ya utalii kimataifa.

“Naelekeza sasa tujipange kuanzia sasa kwa ajili kuandaa tamasha hili la kimataifa la utamaduni na sanaa na tushirikiane na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya nje kulitangaza nje ya mipaka ya nchi yetu na tuwakaribishe wageni.” Amesisitiza Mhe. Waziri

Ameitaka Wizara yake ishirikiane na  Wizara  ya Utalii ili tuweze kuuza  sanaa na Utamaduni nje ya Tanzania kupitia  mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na matamasha  ya utamaduni.

Akitolea mfano amesema TaSUBa inatakiwa kuwa wabunifu kwa kuandaa wa Tamasha la Utamaduni kama tamasha Masai nchini Uingereza na Marekani ili kuuza na kutangaza utamaduni duniani.

Amesema  katika kipindi hiki atahakikisha  masuala ya uzembe, rushwa, ubadhilifu hayana  nafasi  kwenye wizara yake ili kuleta mapinduzi ya haraka kwenye sekta anazozisimamia.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi ametumia  tukio hilo  kutangaza rasmi kuwa  shughuli za TaSUBa  zitakuwa zikisimamiwa  kwa karibu zaidi ya Naibu wake.





Post a Comment

Previous Post Next Post