MHE. MCHENGERWA AELEZA NAMNA RAIS SAMIA ALIVYOIBEBA TASNIA YA FILAMU NCHINI

 Na. John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Omary Mchengerwa amepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuweka mazingira wezeshi ya kuendesha shughuli za sanaa na michezo nchini kwa kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati ambazo zimeanza kuzaa matunda  katika kipindi kifupi. 

Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo, Februari 12, 2022 kwenye dhukuru na wadau wa tasnia ya Filamu iliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amesisitiza kuwa dhamira yake pia ni kuona sekta ninazozisimamia zinapiga hatua kubwa za kimaendeleo, na kuleta mapinduzi makubwa ambayo hayajawai kutokea.  Ametaja baadhi ya mazingira wezeshi ambayo Mhe. Samia ameyaweka katika kipindi hiki kuwa ni pamoja na kuandaa filamu ya Royal Tour inayolenga kuitangaza Tanzania katika Nyanja mbalimbali za uwekezaji ikiwemo katika sekta ya filamu ambayo yeye mwenyewe ameshiriki kikamifu katika filamu hiyo.  

Pia amesema Mhe. Rais ameridhia kutenga fedha za maendeleo ya sanaa na michezo, kiasi cha Shilingi Bilioni 2.5 kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni ambazo   zitawasaidia wasanii kupewa mikopo midogo midogo kwa ajili ya kuandaa kazi zao na kuzirejesha taratibu na bila riba. 

Amesema katika kipindi hiki bajeti ya Wizara yake imeongezeka ili kuiwezesha kukamilisha programu zake za maendeleo na kufikia malengo yake iliyojiwekea, ikiwemo utafutaji masoko ya filamu zinazozalishwa nchini. 

Amefafanua kwamba Wizara tayari imeimarisha mifumo ya urejeshwaji wa faida ya kazi za sanaa kupitia mirabaha, ambapo sekta ya filamu ni miongoni mwa sekta zilizoanza kunufaika. 

Pia  kuimarisha uhusiano wa kimataifa ili kufungua milango nje ya nchi na kutoa fursa kwa bidhaa za kitanzania hususan filamu kuuzika katika soko la kimataifa. 

Kwa upande mwingine amesema Serikali inakwenda kuanzisha programu ya kuzalisha filamu kubwa za kitaifa zitakazokuwa zinafadhiliwa na Serikali mahususi kwa ajili ya kuhifadhi historia, utamaduni, pamoja na kutangaza nchi na kuongeza viwango vya ubora wa filamu zinazozalishwa nchini.

Kununua na Kuanzisha maktaba ya vifaa vya filamu vya kisasa itakayotoa fursa kwa wadau kupata vifaa bora na kwa gharama nafuu ili kuboresha filamu zinazoandaliwa nchini. 

Kuhusu kilio cha muda mrefu cha waandaji wa filamu Mhe Mchengerwa amesema Wizara inakwenda kuandaa mwongozo kwa wanunuzi wa filamu hapa nchini kununua filamu hizo kwa bei inayomfaidisha mwandaaji wa filamu hiyo pamoja na wasanii kiujumla.  

Amesema Serikali itajenga jijini dodoma jengo la kisasa  ikiwa ni kitega uchumi kwa ajili ya kuwezesha mfuko wa sanii na kutoa huduma za pamoja (One Stop Service Centre) pia  nyumba zenye hadhi na kwa gharama nafuu wasanii ili kulinda heshima na hadhi ya wasanii.

Naye Katibu Mkuu Dkt. Hassani Abbasi amemshukuru Mhe. Mchengerwa  kwa kuongoza kikao hicho kwa mafanikio makubwa  huku akifafanua kuwa  kila upande unamambo ya kuyatekeleza ambapo kwa upande wa Wizara amemwagiza  Mkurugenzi wa Sanaa kuyaainisha yote na kuyapatia ufiumbuzi mara moja. 

Awali Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu nchini Kiagho Kilonzo  amesema  tasnia ya filamu imekuwa ikikua kila kukicha  hivyo ushirikiano wa wadau wote ni muhimu kufikia mapinduzi ya kweli ya filamu nchini. Wakichangia kwa nyakati tofauti wadau hao wamempongeza Waziri Mchengerwa kwa ubunifu wa kuwa na dhukuru na wadau ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zao kwa pamoja.





Post a Comment

Previous Post Next Post