NAIBU WAZIRI MALIASILI AHIMIZA UHIFADHI WA MISITU

  Naibu Waziri wa Maliasili na Utaliii Mhe. Mary Masanja ametoa rai kwa viongozi wa Kanda ya Ziwa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa mazingira hususan katika mkoa wa Mwanza na Simiyu, lengo likiwa ni kuboresha maisha ya kila kiumbe ya sasa na siku za usoni.

 Rai hiyo imetolewa leo mara baada ya kupokea taarifa ya Hali ya Uhifadhi  mkoani Mwanza ambapo Waziri alizitaka jamii za wakulima na wafugaji zinazoishi maeneo ya Hifadhi za Misitu ziishi kwa amani na kuhifadhi mazingira kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.

 Mhe. Masanja anasema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wananchi wa vijiji vinavyouzunguka msitu nchini ni elimu juu ya uhifadhi na athari zake, namna wanavyoweza kutumia hifadhi za misitu kutokomeza umaskini pamoja na kutokuwepo na matumizi bora ya ardhi.

 Kufuatia hali hiyo, Waziri ametoa rai kwa uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS, viongozi wa Wilaya na Vijiji kushirikiana pamoja kuelimisha wananchi wanaozungumza hifadhi za misitu huku Wakala ukitakiwa kutafuta miradi kupitia programu za kurudisha kwa jamii (CSR) kusaidia jamii kando mwa misitu.

 “Ninafahamu kuwa kuna Kamati ya Mawaziri nane iliyoundwa kushughulikia migogoro ya mipaka katika hifadhi yza misitu, lakini wakati tukishubiri kamati hiyo kutoa mapendekezo yake, tuanze sasa kutoa elimu na kuwafanyia vitu vingi vya CSR ikiwemo kuwapelekea miradi ya Ufugaji Nyuki pamoja na Kilimo na Ufugaji bora ili watuelewe, na wajue tunapohimiza uhifadhi tuna lengo zuri,” anasema Mhe. Masanja.

 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel anasema misitu iliyopo Kanda ya Ziwa haina hali nzuri na kuwataka viongozi kuchukua hatua za kuhimiza uhifadhi.

 “Msitu yetu tumeiona kwenye ramani kubwa ya Kanda ya Ziwa hapa, niwaombe viongozi tuwe na moyo wa kihifadhi, kanda hii kuna maeneo yalikuwa na mvua mara mbili kwa mwaka na sasa mvua ni zakubahatisha huku maeneo mengine yakikumbwa na ukame, hakuna muujiza ni uhifadhi. Kuna maeneo yalikuwa na mito mikubwa sasa imekauka na ng’ombe wamekufa, tuna haja kubwa yakuwekeza kwenye mabadiriko ya tabia nchi,” anasema Mhe.  Mkuu wa Mkoa.

 Anaongeza kwa kusema kuwa “viongozi wote kwa pamoja tuwe na wimbo mmoja, waheshimiwa wabunge, viongozi wa Serikali Kuu, taasisi za umma na binafsi tushirikiane sote kwa pamoja tuhifadhi misitu yetu kwa faida ya kizazi kijacho ambacho tusipofanya maamuzi magumu leo hii hakitakuwa na furaha, tusiwe wabinafsi.” 

 Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe.  Salum Kali, Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria na wabunge wawakilishi wa wananchi wanaoishi kando mwa hifadhi za misitu walisema, uhifadhi nchini una faida kubwa, muhimu ni kuwepo na programu ya kutoa mafuzo ya uhifadhi sambamba na kuanzisha miradi yenye manufaa katika uhifadhi wa misitu na kuleta manufaa kwa wananchi.

 Awali Kamishna wa Uhifadhi – TFS Prof. Dos Santos Silayo alisema Wakala uko tayari kushirikiana na viongozi wa Kanda ya Ziwa katika kuhakikisha kuhakikisha uhifadhi unafanikiwa.

 Aidha alisisitiza  kuwa licha ya changamoto mbalimbali za uhifadhi nchini, Wakala utaendelea kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki ili kuchangia kikamilifu mahitaji ya kijamii, kiuchumi, kiikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.



Post a Comment

Previous Post Next Post