WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme hususan maeneo ya vijijini ambapo hadi sasa jumla ya vijiji 10,361 kati ya vijiji 12,317 vya Tanzania Bara sawa na asilimia 84.12 vimeunganishiwa umeme.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha hadi kufikia Desemba 2022 vijiji 1,956 vilivyosalia vinapata umeme kupitia Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ulioanza kutekelezwa Julai, mwaka huu. Gharama za mradi huu ni shilingi trilioni 1.24.”
Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Novemba 12, 2021) wakati akiahirisha Mkutano wa tano wa Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma. Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji na usambazaji umeme maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha maeneo yote ya mijini na vijijini yanapata umeme wa kutosha, nafuu na uhakika.
Mheshimiwa Majaliwa ametaja baadhi ya miradi ya kimkakati ya uzalishaji umeme kuwa ni mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (MW 2,115) ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 55.6 na mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rusumo (MW 80) uliofikia asilimia 81.2.
Vilevile, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imekamilisha mradi wa njia ya kusafirisha umeme (KV 220) kutoka Bulyanhulu hadi Geita wenye urefu wa kilomita 55. Miradi mingine ya kusafirisha umeme inayoendelea kutekelezwa ni kutoka Rusumo kwenda Nyakanazi kupitia Benaco (KV220), Tabora kupitia Urambo - Nguruka hadi Kidahwe (KV 132) na Tabora hadi Katavi kupitia Ipole na Inyonga (KV132).
“…Serikali inaendelea na maandalizi ya mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Iringa – Mbeya – Tunduma hadi Sumbawanga na mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa KV 400 kutoka Sumbawanga – Mpanda hadi Kigoma.”
Amesema kukamilika kwa miradi hiyo ya uzalishaji na usambazaji umeme kutawezesha maeneo yote nchini kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa na hivyo kupata huduma ya uhakika ya umeme.