Afisa Usalama wa Chakula Mwandamizi wa TBS, Bi.Imakulata Justin akizungumza na waandishi wa habari leo kuelekea Siku ya Chakula Salama Duniani, katika ofisi za Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam kuelekea Siku ya Chakula Salama Duniani ambayo hufanyika June 7 kila mwaka. Afisa Usalama wa Chakula Daraja la kwanza TBS, Bw.Kaiza Kilango akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam kuelekea Siku ya Chakula Salama Duniani ambayo hufanyika June 7 kila mwaka.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
*****************************
NA EMMANUEL MBATILO
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Chakula Salama Duniani, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wazalishaji wa vyakula kuandaa vyakula katika hali salama yakiwemo mazingira salama ili kuweza kumlinda mlaji asiweze kupata madhara ya kiafya.
Kauli mbiu ya mwaka huu kuelekea Siku ya Chakula Salama ambayo huadhimishwa kila mwaka June 7 ni “CHAKULA SALAMA LEO KWA AFYA NJEMA KESHO”.
Ameyasema hayo leo Afisa Usalama wa Chakula Mwandamizi wa TBS, Bi.Imakulata Justin akizungumza kuelekea Siku ya Chakula Salama Duniani, katika ofisi za Makao Makuu ya TBS Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Bi.Imakulata amesema mazingira ya pale wanapozalisha vyakula kunahitajika kuwa safi na salama ili kuhakikisha kile chakula kinachozalishwa ni salama.
“Unapofanya biashara ya chakula basi unatakiwa kuhakikisha chakula hicho kinakuwa katika hali ambayo haiatarishi usalama wa chakula husika mfano kuna chakula kinatakiwa kuwekwa kwenye hali ya ubaridi basi kiwekwe hivyo au kinatakiwa kuhifadhiwa katika sehemu kavu basi kifanyiwe hivyo”. Amesema Bi.Imakulata.
Aidha Bi.Imakulata amesema kuwa mtayarishaji wa pombe za kienyeji anatakiwa kuhakikisha marighafi ambazo hutumia kutengeneza pombe ni salama.
Pamoja na hayo amesema jukumu la TBS ni kuhakikisha chakula kinachozunguka katika masoko ni salama hivyo hufanya kaguzi mbalimbali katika masoko kuhakikisha kwamba kile kinachouzwa ni salama kwaajili ya afya ya mlaji.
Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula Daraja la kwanza TBS, Bw.Kaiza Kilango amesema wakulima wanayo nafasi kubwa ya kufanya kuhakikisha kwamba sumu zinazotumika kudhibiti wadudu mashambani zinatumika kwa kuzingatia kanuni za usalama wa chakula.
“Mkulima anapoweka sumu kwenye mbogamboga au kwenye nyanya lazima apate ufafanuzi wa ile sumu inavyotumika kutoka kwa afisa ugani aliyekaribu nae na apate ufafanuzi namna gani inavyotumika na chakula kiwe tayari kuvunwa kwa matumizi ya binadamu”. Amesema Bw.Kilango.