TIC YASHAURI TAASISI ZA SERIKALI KUENDELEA KUISAIDIA KAMPUNI YA ALPHAKRUST, MAFIA

 Kutoka kushoto ni Afisa mdhibiti ubora wa kampuni ya Alphakrust Mr. Tarun, Nestory Kissima (Afisa kutoka TIC), Daudi Riganda (Meneja kutoka TIC), Girson Ntimba (Mchumi kutoka TIC) na Bw. Stephen (Msimamizi wa Mashamba ya uvuvi wa Samaki) wakiwa eneo lenye mabwawa 36 ya Samaki katika kijiji cha Jimbo wilaya ya Mafia.

Maafisa kutoka Kituo cha Uwekezaji wakioneshwa Samaki wachanga ndani ya mojawapo ya mabwawa yanayotumika kufugia Samaki aina ya kamba yaliyopo katika kijiji cha Jimbo wilaya ya mafia.

*********************

Wafanyakazi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiongozwa na Meneja wa Kituo hicho Bw. Daudi Riganda wamefanya ziara ya kutembelea mradi wa ufugaji wa samaki aina ya kamba na kiwanda cha kuchakata samaki wa aina zote kwa ajili ya soko la nje wilayani Mafia.

Mradi huu unamilikiwa na kampuni ya Alphakrust ambayo wamiliki wake ni watanzania wenye asili ya bara la Asia kwa asilimia 100.

Katika ziara hiyo wameambatana na maafisa wengine ambao ni Bw. Riganda pamoja na Grison Ntimba na Nestory Kissima. Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kuangalia maendeleo na changamoto za mradi huo.

Aidha, Timu hii kutoka TIC ilikuwa inaangalia namna mkataba wa uwekezaji (performance contract) wa mradi huo mahiri ulivyozingatiwa.

Mradi huu uliandikishwa kama mradi wa kimkakati na kupewa hadhi ya uwekezaji mahiri tarehe 9 Septemba 2010 kwa ajili ya kuanzisha na kuendesha mradi wa ufugaji wa samaki aina ya kamba (prawns) kwa ajili ya soko la nje.

Akizungumzia maendeleo ya mradi huo na namna mkataba wa uwekezaji (performance contract) ulivyozingatiwa, mwakilishi wa kampuni ya Alphakrust ambaye pia ni Quality Controller Bw. Tarun, alisema hadi kufikia mwaka huu 2021 wamefanikiwa kuwekeza jumla ya Shilingi bilioni 22.490 katika mradi huu katika ujenzi wa mashamba la samaki, sehemu ya kuzalishia na kukuzia vifaranga vya samaki (hatchery) na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata samaki kwa ajili ya soko la nje.

Kiwango cha uwekezaji huu ni zaidi ya kile kilichotajwa katika mkataba wa uwekezaji (performance contract) ambapo kiasi cha shilingi bilioni 21.5 kilikadiriwa kuwekezwa kupitia mradi huu.

Kwa muda wa zaidi ya miaka 7 hadi 8 wawekezaji wa kampuni hii wamekuwa wakizalisha mbegu za vifaranga vya samaki na kufikia milioni 27.

Hata hivyo kwa kipindi cha miaka 3 iliyopita uzalishaji wa mbegu hizi umekuwa ukishuka kutokana na ucheleweshwaji wa vibali vya kuruhusu ukusanywaji wa samaki wazazi (brood stock) kutoka Serikalini kupitia Wizara ya Uvuvi, hali inayoathiri sana maendeleo ya mradi huu.
 
Mafanikio mengine yaliyoripotiwa kwenye Timu ya TIC kupitia uwekezaji wa kampuni ya Alphakrust ni pamoja na ujenzi wa shamba la samaki katika eneo la Site A katika kijiji cha Jimbo wilaya ya Mafia ambao umekamilika.

Eneo hili lenye maji lina jumla ya hekta 60.63 na tayari limeanza kufanya kazi. Hadi hivi sasa jumla ya mabwawa ya samaki 36 yamejengwa yakiwa na uwezo wa kuvuna samaki aina ya kamba 5,000 kwa wastani kwa hekta kila baada ya kipindi cha siku 150.

Aidha, kati ya mwaka 2011 na 2016 uzalishaji wa samaki ulifikia tani 361 kwa mwaka. Hata hivyo mwaka 2017, 2018, 2019 na 2020 uzalishaji ulishuka kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na ruhusa ya kuingiza mbegu za samaki wazazi (brood stock) kuchelewa kutolewa na Wizara ya Uvuvi.

Akizungumza kwa niaba ya Timu ya TIC, Bw. Riganda alisema wamefurahishwa na namna uzalishaji wa samaki katika mabwawa na kiwandani unavyozingatia viwango vya Umoja wa Ulaya (EU) na hivyo kufanikisha kupata masoko katika nchi za umoja wa ulaya.

Karibu asilimia 80 ya masoko ya samaki wanaozalishwa kupitia mradi huu yapo Ufaransa, huku Ureno na Italia zikichukua asilimia 20 iliyobaki.

Timu kutoka TIC ilifurahishwa pia uwekezaji uliofanyika kwenye vifaa vya kisasa vya upozaji (freezing equipment) na barafu vilivyomo kiwandani.

Jumla ya ajira za moja kwa moja zipatazo 263 zimetengenezwa kupitia uwekezaji huu. Aidha, katika uwekezaji huu, kampuni ya Alphakrust iliweza kupata mapato kupitia mauzo ya nje hali iliyowezesha serikali pia kupata fedha za kigeni.
 
Hata hivyo, licha ya mchango wa kampuni hii katika maendeleo ya jamii na kiuchumi kuna changamoto kadhaa ambazo zinaikabili. Changamoto hizo ni pamoja na mkataba wa ukodishaji baina mwekezaji na Wizara ya Uvuvi kuelekea ukomoni kwani unaisha mwaka 2023.

Aidha, wawekezaji wanalalamikia ucheleweshwaji wa vibali vya kuruhusu ukusanywaji wa samaki wazazi (brood stock) kutoka Serikalini kupitia Wizara ya Uvuvi, hali inayoathiri sana maendeleo ya mradi huu.
 
Timu ya TIC ilichukua changamoto hizo ili kuziwasilisha katika mamlaka ya ngazi za juu huku mapendekezo yao yakiwa ni serikali kupitia Wizara ya Uvuvi kuangalia uwezekano wa kuwaongezea wawekezaji muda zaidi kwenye mkataba wao kutokana na umuhimu wa mradi huo kwa taifa; Serikali kupitia Wizara ya Uvuvi kuangalia uwezekano wa kutoa kibali kimoja cha ukusanyaji wa samaki wazazi (brood stock) kwa mwaka mzima tofauti na inavyofanyika hivi sasa; na Serikali kuendelea kuwapatia ushirikiano wawekezaji hawa ili wazalishe zaidi kwa ajili ya soko la nje ili kupata mapato ya fedha za kigeni.
 
Miradi ya kimkakati kwa wawekezaji mahiri imezungumziwa kwenye Sehemu ya 20 ya Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 na Sehemu ya 49 ya Kanuni za Uwekezaji za mwaka 2002, kama miradi mikubwa na yenye mitaji mikubwa ambayo sheria hizo zinairuhusu kufaidi au kupata vivutio zaidi ya vile ambavyo vinatolewa kwa wawekezaji wa kawaida.

Sheria inawataka wawekezaji mahiri ambao ni watanzania kuwa na mitaji ambayo haipungui Dola za Kimarekani milioni 20 kwenye uwekezaji watakaoufanya, na kwa wale raia wa kigeni wanatakiwa kuwa mitaji ambayo haipungui Dola za Kimarekani milioni 50 kwenye uwekezaji watakaoufanya.

Aidha, kuna wawekezaji mahiri maalum (special strategic investors) ambao mitaji yao inatakiwa isipungue Dola za Kimarekani milioni 300.

Miradi yote hii inasimamiwa na Kamati Maalum ya Kitaifa ya Uwekezaji ikiwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu na katibu akiwa ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Wajumbe wengine katika Kamati hii ni pamoja na Waziri wa Fedha, Waziri wa Uwekezaji, Waziri wa Ardhi, Waziri wa Serikali za Mitaa, Waziri wa Kilimo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Post a Comment

Previous Post Next Post