FANYENI KAZI KWA UADILIFU NA UAMINIFU – KASEKENYA

 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, akiongea na baadhi ya watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi mkoani Manyara (hawapo pichani), kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Manyara. Pembeni yake ni Meneja wa TANROADS Manyara, Mhandisi Bashiri Rwesingisa. 

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Manyara, Mhandisi Bashir Rwesingisa akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa pili kushoto), wakati wa kikao cha Naibu Waziri huyo na baadhi ya watumishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TANROADS Manyara. 

Meneja wa Wakala Ufundi na Umeme (TEMESA) Manyara, Mhandisi Margareth Julian, akifafanua jambo Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa kwanza kushoto), wakati wa kikao cha Naibu Waziri huyo na baadhi ya watumishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TANROADS Manyara.  

Baadhi ya watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (hayupo pichani), kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TANROADS mkoani Manyara. 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya (wa nne kutokea kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa taasisi zilizochini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi mkoani Manyara, baada ya kufanya kikao na watumishi hao.

**************************************

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi mkoani Manyara kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na taaluma zao ili kuongeza ufanisi.

Akizungumza na baadhi ya watumishi hao mara baada ya kumaliza ziara yake siku mbili mkoani humo, Mhandisi Kasekenya amewataka watumishi wa taasisi hizo kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya taaluma zao ili kuleta matokeo yenye tija na yanayopimika.

“Inaumiza sana kuona wataalamu walioaminiwa na serikali wakitekeleza majukumu yao chini ya kiwango, sitakua tayari kutetea uovu, inawapasa mbadilike kwa kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi ili kuleta tofauti yenye tija” alisema mhandisi Kasekenya.

Aliongeza kuwa gharama za matengenezo ya magari ya serikali zinazotozwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) ni kubwa mno na kuwataka TEMESA kubadilisha mtazamo wa kazi kwa kusikiliza maoni ya wateja wao pamoja na kuwa gharama za matengenezo ya magari zinazoendana na bei ya soko.

Hata hivyo Naibu Waziri Kasekenya alipongeza juhudi zinazofanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani humo, kwa kuhakikisha kuwa barabara zote wanazo zisimamia zinapitika katika majira yote ya mwaka.

Akisoma taarifa ya utendaji kazi, Meneja wa TANROADS Manyara Mhandisi Bashiri Rwesingisa alizitaja changamoto mbali mbali wanazopambana nazo ikiwa ni pamoja na kupanda kwa bei ya nondo na saruji, upungufu wa kokoto kwa ajili ya kazi za barabara na madaraja, pamoja na ukosefu wa wakandarasi wenye uwezo. na uzoefu wa kazi za madaraja.

Nae Meneja wa TEMESA Manyara Mhandisi Margareth Julian, alimuambia Naibu Waziri Kasekenya kuwa, ofisi yake inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi pamoja na kuwa na mzigo mkubwa wa madeni ambayo taasisi hiyo inawadai wateja wake kutokana na huduma ya matengenezo ya magari wanayoitoa, lakini pia kushindwa kulipa kwa wakati madeni wanayodaiwa na wazabuni.

Mhandisi Kasekenya alikuwa mkoani Manyara kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kukagua barabara za Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu Kilometa 50.5, Mbulu hadi Haydom Kilometa 81, Mugitu hadi Haydom Kilometa 68.35 na Singe kwenda Kimotorok hadi Sukuro Kilometa 155, zinazoombewa fedha na wabunge wa Mbulu Mjini, Mbulu Vijijini, Hanang, Babati Mjini na Babati Vijijini ili ziweze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Imetolewa na, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post