Na Chalila Kibuda ,Chalinze
NAIBU Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Andrea amemwagiza Mkuu wa Kanda ya Mashariki wa Mamlaka Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Lawi Odiero kushughulikia haraka maombi ya Halmashauri ya Chalinze ya kuimarisha Miundombinu ya mawasiliano ikiwemo kupatiwa maombi ya uanzishaji wa radio na Televisheni katika Halmashauri hiyo ambayo yalikwama kwa muda mrefu.
Pamoja na maombi hayo ziara ya Naibu Waziri huyo ilikuwa kuangalia huduma ya Mawasiliano katika Halmashauri ya Chalinze na changamoto wanazokuta nazo wakati wa kufanya mawasiliano.
Naibu Waziri Mhandisi Kundo ameyasema hayo wakati wa ziara maalum alipofanya ziara katika Halmashauri hiyo ya Chalinze ikiwa ni muendelezo wa ziara yake anayoendelea nayo Nchini kuangalia hali ya mawasiliano nchini.
Naibu Waziri aliongozana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Kampuni za Simu za Mkononi kuweza kutoa ufafanunuzi katika maeneo yanayowahusu.
Amesema vijiji 1057 vimefikiwa na huduma za mawasiliano ya simu hivyo tunakwenda katika uchumi wa Kisasa wa kutoka kwenye Barabara na kutumia simu na kuchangia pato la Taifa.
Amesema mawasiliano ya simu kwa kuwasiliana au kutumia data sio anasa tena kwani uchumi ndio unakwenda huko na serikali ni kuhakikisha tunafikisha huduma ya Mawasiliano.
Kwa upande wake Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete alimueleza Naibu Waziri kuwa uimara wa mawasiliano ni pamoja na kupata vyombo vya mawasiliano kama Redio na Televisheni ili kuwezesha upashanaji wa habari ya mazuri yanayofanyika katika Wilaya hiyo na hata Tanzania kwa jumla. Katika kuimarisha mawasiliano Mhandisi Kundo amebainisha kuwa, kukosekana kwa radio hiyo inasababisha Wananchi kushindwa kusikia mambo mazuri yanayofanywa na Serikali yao chini ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
"Wananchi wanataka kusikia mambo yanayofanywa kwenye Halmashauri yao. Pia wanataka kusikia Diwani wao kafanya nini au Mbunge wao kafanya jambo gani ili kupunguza maswali wakati wa kazi au kwenye mikutano ya viongozi wao ama kwa serikali yao." Alisema Mhandisi Kundo.
Aidha, Mhandisi Kundo alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mbunge wa Chalinze kwa kuwa mtu wa mstari katika kupigania maendeleo ya jimbo hilo. Naibu Waziri alieleza kuwa, alipokea taarifa kwa Mbunge wa Jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete juu ya ombi la uchelewashwaji wa frequency za Radio hiyo ya Halmashauri ya Chalinze, hivyo ameamua kutembelea pamoja na shughuli nyengine za kiserikali, kujionea uhalisia sambamba na matatizo mengine ya kimawasiliano.
"Mbunge wetu Ridhiwani Kikwete aliniuliza juu ya tulipofikia suala lao la Radio frequency. Kiukweli suala ili nimelijua jana na leo nimefika hapa hivyo basi ninamwagiza Mkuu wa Kanda wa Mashariki wa TCRA ambaye yupo hapa ahakikishe analifanyia kazi na hadi jioni ya leo niwe nimepata majibu ya kurejesha kwa Mbunge’ amesema Mhandisi Kundo.
Aidha, akijibu suala la changamoto ya upatikanaji hafifu wa mawasiliano baadhi ya maeneo ya Jimbo hilo, Naibu Waziri alibainisha kuwa, kumekuwa na changamoto wa usimikwaji wa minara ya Mawasiliano baadhi ya maeno ikiwemo pia changamoto wa upatikanaji wa vibali.
"Vibali vimekuwa vikichukua muda mrefu kuanzia miezi mitatu hadi Sita. Kuna wenzetu wa Mazingira NEMC ambao wao wanachukua hadi miezi Sita, lakini pia Mamlaka ya anga, watu wa hali ya hewa na wadau wengine. Lakini nina hakika masuala haya yatafanyiwa kazi na mawasiliano yatakuwa vizuri" alisema Mhandisi Kundo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo, Ridhiwani Kikwete alimshukuru Naibu Waziri kwa kufika jimboni Chalinze pamoja na kukubali maombi yao ya kuhakikishiwa mazingira bora ya mawasiliano.
Ridhiwani alimshukuru Naibu Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchagua viongozi wachapa kazi kama Mhandisi Kundo ambaye amekuwa akifika majimboni kutatua kero za wananchi.
"Naibu Waziri leo umekuja hapa Jimboni utatupatia mwanga mpya kupitia mawasiliano yetu. Jimbo letu limekuwa na shida katika mawasiliano kwa muda mrefu matatizo ambayo yana sura zinazofanana katika utatu wake." Alisema Ridhiwani Kikwete.
Akieleza juu ya shida hiyo Mbunge Ridhiwani Kikwete alitoa mfano wa kijiji cha Matipwili na Kijiji cha Mkoko, alieleza shida kubwa ya vijiji vyote zinafanana ambapo mitambo hiyo uzimwa inapofika saa mbili au nne usiku hivyo wananchi kukosa mawasiliano usiku.
Hata hivyo akijibu Meneja wa Kampuni ya Tigo ambao ndiyo wanaosimamia mradi huo, alikiri juu ya tatizo hilo lakini sasa limerekebishwa kwa kurekebisha miundombinu na mazingira ya kuwapatia wananchi mawasiliano.
Pamoja na hilo Mbunge alieleza matatizo mengine yakiwemo yale ya mawasiliano kukosekana barabarani kati ya kijiji na kijiji au miji na miji mfano kijiji cha kwa Mduma na Kitongoji cha Gole, Alibainisha Mbunge Ridhiwani Kikwete.
Akijibu, Naibu Waziri alimuhakikishia Mbunge na wananchi wa Chalinze kuwa Serikali inaangalia pia thamani ya biashara na kupitia Mfuko wa mawasiliano kwa Umma mapungufu kama haya yanaangaliwa na kufanyiwa kazi.