SERIKALI YABAINI MPANGO KUKWAMISHA UJENZI WA VIWANDA VYA SUKARI-PROF. MKENDA

 

*******************************************

SERIKALI imebaini uwepo wa mkakati wa kukwamisha kuanza kwa ujenzi wa viwanda vingi vya kuchakata miwa ya wakulima ili nchi isijitosheleze kwa uzalishaji wa sukari nchini.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa leo (17.02.2021) na Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda wakati akiongea na wakulima wa miwa wa bonde la Mbigiri wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro ambapo ameeleza kuwa bado wamiliki wa viwanda vya kuzalisha sukari vilivyopo nchini wameshindwa kununua miwa yote ya wakulima

Waziri huyo amesema kuwa kuna taarifa za uhakika kuwa baadhi ya watu wasioitakia mema nchi wanakwamisha jitihada za kuanzishwa kwa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Mkulazi II hatua ambayo inayoendelea kuwaumiza wakulima wa miwa kwa mazao yao kutupwa kwa kukosa wanunuzi wa uhakika

“Nawahakikishia ninazo taarifa kwamba sasa kiwanda kitakamilika na kuanza kazi haraka, kwa hiyo wakulima msiwe na wasiwasi na soko la miwa. Anayezuia kiwanda hiki cha Mkulazi II kisianze kazi serikali itachukua hatua kali. Tunawashukuru wakulima kwa uvumilivu wenu, serikali haitawaangusha” alisema Prof. Mkenda

Kwa muda wa miaka mitatu sasa tangu mwaka 2018 wakulima wa miwa wa Bonde la Mbigiri wilaya ya Kilosa wamekuwa wakihangaika kuuza miwa yao kutokana na kiwanda cha Mkulazi kushindwa kukamilika huku wakulima wakiendelea kudaiwa mikopo ya fedha walizokopeshwa na Benki ya Azania

Katika hatua nyingine Waziri Mkenda ametoa onyo kwa wawekezaji wa viwanda vya sukari Kilombero na Mtibwa kuondoa zuio la wakulima kuuza miwa yao kwa watu wengine kwa kigezo cha kulinda soko la ndani hatua inayosababisha wakulima miwa kukosa soko na nchi kuendelea kuwa na upungufu mkubwa wa sukari.

Waziri Mkenda aliongeza kuwa wizara itaangali upya marufuka hiyo ya kuzuia wakulima kuuza miwa inayowapa nafuu kampuni za Kilombero na Mtibwa pekee kuwa wanunuzi wa miwa ya wakulima hivyo wafanyabiashara wengine wenye nia ya kununua miwa kushindwa. Amesema kunapokuwa na wanunuzi wengi wa miwa kunaleta nafuu kwa wakulima ambao huchagua nani wamuuzie miwa na kuongeza ushindani wa bei katika soko

“Leo mkulima wa miwa hana soko la uhakika alafu Mtibwa Sugar anataka serikali imlinde wakati  tunahitaji maslahi mapana kwa wakulima wetu. Kazi yangu kama Waziri wa Kilimo ni kumlinda mkulima, siwezi kulinda marufuku ya kuzuia miwa popote iendelee, tutachukua hatua . Kwanini tumzuie mkulima auze miwa yake popote” alisisitiza Waziri Mkenda.

Prof.Mkenda amehoji “ ni uchumi gani kumzuia mkulima auze miwa yake kwa mtu anayetaka kununua halafu mwekezaji anataka serikali imlinde wakati yeye hanunui na zaidi ya tani 350,000 za miwa huharibika mashambani “ kisha akawataka wakulima wa Kilosa na Mvomero kuwa na subira wakati mkakati wa kuanzisha kiwanda cha Mkulazi ukikamilika.

Wakulima wa miwa wa kijiji cha Mbigiri walimweleza waziri huyo kuwa kutokuanza kwa kiwanda cha sukari cha Mkulazi kumesababisha washindwe kurejesha mikopo walipopewa na benki ya Azania mwaka 2018 na kuwa sasa imefikia wanadaiwa riba ya asilimia 6 ikiwa ni adhabu kwa Kuchelewa kurejesha asilimia 50 ya mikopo.

“Sasa imefika wakati mkandarasi aliyetulimia mashamba anadai fedha za kulima ambapo ametuzuia tusivune miwa yetu. Tunaomba wizara isaidie mkandarasi aliyepewa kazi na kampuni ya Mkulazi alipwe fedha zake  ili na sisi turuhusiwe kuvuna mashamba yetu” alilalamika Godfery Philipo mkulima wa miwa wa Mbigili.

Naye  Mkulima Saidi Mazunde wa Mbigiri alisema tatizo la kudaiwa kukatwa riba ya asilimia sita zaidi limetokana a mkataba kati ya Kampuni ya Mkulazi , AMCOS na wakulima kuwa kitakapoanza kiwanda wakulima wote watauza miwa yao huko .Sasa ni miaka mitatu kiwanda hakijaanza  na mkulima anaonekana kupewa adhabu.

“ Hii asilimia 6 ya riba ya adhabu tunaomba ibebwe na Mkulazi kwa kuwa ndio waliotushawishi tulime kwa kuwa wataanzisha kiwanda hapa Mbigiri” alisema Mazunde.

Kwa upande wake Mwenyekiyi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Dkt. Chritine Ishengoma alisema wakulima wasikate tamaa na kuacha kulima miwa kutokana na kiwanda Kuchelewa kuanza bali wawe watulimvu kwa kuwa seriklai ya awamu ya tano imepokea kilio chao kwa Waziri wa Kilimo kuja kuwasilikiza .

“Wakulima wangu msife moyo mkachukua hatua za kuchimbua miwa,Tunataka kilimo kimkomboe mkulima hivyo kwero zenu zitapatiwa ufumbuzi haraka.” Dkt. Ishengoma

Prof. Mkenda akihitmisha ziara yake mkoa wa Morogoro leo ameiagiza Bodi ya Sukari nchini kukutana na viwanda vya sukari vyote nchini kuweka utaratibu wa kupima viwango vya utamu wa sukari kutumika kuuzia miwa badala ya matumizi ya mizani hatua inayolalamikiwa na wakulima .

Pili ametoa rai kwa taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kutoa mikopo kwa wawekezaji wa ndani wenye nia ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kuchakata miwa na kuzalisha sukari hatua itakaoondoa utegemezi wa viwanda vikubwa vya sukari.

Na tatu,wizara itafanyia kazi marufuku ya kuuza miwa nje ya eneo la mwekezaji iliyopo hatua inayodidimiza jitihada za serikali kukuza uzalishaji wa miwa kwani imeonekana ni njama ya kuwaumiza wakulima na kupeleleka miwa kuharibika shambani bila soko.

Waziri Mkenda amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Morogoro leo amabpo alitembelea vowanda vuya sukari vya Kilombero, Mtibwa na  skimu za umwagiliaji Msolwa Ujamaa pamoja na kukongea na wakulima wa miwa kwenye wilaya za Kilombero, Mvomero, Kilosa na Morogoro.

Post a Comment

Previous Post Next Post