Naibu
Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro anayesimamia (Uhifadhi,
Utalii na Maendeleo ya Jamii) Dkt. Christopher Timbuka amewapongeza
wananchi waliohamasika na mradi wa shamba la Mang’ola juu Wilayani
Karatu lililoanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanaoishi ndani
ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Dkt Timbuka amesema hayo leo tarehe 19
februari, 2021 wakati akikagua shamba hilo lenye ukubwa wa ekari 53
ambalo NCAA ilisaidia upatikanaji wake kwa lengo la kuwasaidia wananchi
waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kukodi na kulima mazao
mbalimbali ikiwemo mahindi na Maharage kwa ajili ya kuwawezesha kupata
Chakula.
“Kwa kuwa Sheria hairuhusu kulima ndani ya Hifadhi,
Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ilitafuta eneo hili
nje ya Hifadhi ili Wananchi waweze kukodi na kulima mazao mbalimbali
yatakayowawezesha kupata chakula na kuepuka kutegemea mifugo pekee,
mradi huu ndio umeanza msimu huu na kadri unavyoendelea tunaamini
wananchi wengi watahamasika kulima kwa kuwa eneo lipo la kutosha”
alisema Dkt Timbuka.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi mwandamizi
anayesimamia Idara ya Maendeleo ya Jamii Bw. Mdala Fedes ameeleza kuwa,
mradi huo ulianza kwa kutoa elimu na hamasa kwa Wananchi wa vijiji 25
vilivyopo ndani ya Hifadhi juu ya uwepo wa fursa hiyo ambapo wananchi
246 kutoka vijiji mbalimbali ikiwemo Sendui, Bulati, Misigyo na Olpiro
walikubali kuanza kulima na tayari kati ya ekari 53 zilizolimwa msimu
huu, ekari 47 tayari zimeshapandwa mazao mbalimbali.
“Lengo letu
ni kutoa hamasa zaidi kwa wananchi na tumewaunganisha na wataalam wa
kilimo ili waelimishwe kulima kitaalam na kupata mazao ya kutosha kuliko
kutegemea Serikali moja kwa moja, lengo letu ni kuhakikisha kuwa
mwakani hali ya hewa ikiruhusu wananchi walime ekari 500 kwa kuwa eneo
lipo la kutosha” aliongeza Mdalla.
Mwenyekiti wa Kijiji cha
Sendui kata ya Alaelelai Wilaya ya Ngorongoro Bw. Meeli Saruni
ameishukuru Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuwasaidia kupata eneo
hilo na kuahidi kuhamasisha wananchi wa vijiji vingine waweze
kujitokeza kwa wingi.
Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka (Kulia) akisikiliza maelezo kuhusu mradi wa shamba la Mang’ola kutoka kwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi (Maendeleo ya Jamii) Bw. Mdalla Fedes.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sendui Wilayani Ngorongoro Bw. Meeli Saruni akimuelezea Naibu Kamishna Dkt Timbuka jinsi wananchi wake walivyopokea mradi wa kilimo katika shamba lililoko Mang’ola juu Wilayani Karatu.
Naibu Kamishna wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka (Kulia) akitoa maelekezo kwa watumishi wa Idara ya Maendeleo ya jamii kuhakikisha kuwa wanashirikiana na wananchi wanaolima eneo hilo hasa katika udhibiti wa Wanyamapori wanaongia kwenye mashamba ya wananchi wanaolima nje ya Hifadhi.
Sehemu ya Shamba ambalo wananchi kutoka Kijiji cha Sendui Wilayani Ngorongoro wamelima na kupanda mazao ya Mahindi na Maharage.