SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo imezishauri Taasisi za Fedha kutoa mikopo kwa wawekezaji wanaotaka kuanzisha viwanda vya sukari vikubwa na vidogo ili kuleta ushindani wa soko na lengo la kujitosheleza kwa sukari nchini.
Waziri wa Kilimo , Profesa Adolf Mkenda alisema hayo juzi ( Feb 16) wakati wa ziara ya kikazi wilayani Mvomero, mkoani Morogoro iliyokuwa na lengo la kukagua miradi ya umwagiliaji na hali ya uzalishaji sukari kwenye kiwanda cha Mtibwa , na kuongea na wakulima.
Profesa Mkenda , alisema tayari mkakati wa kuona uzalishaji sukari unaongezeka ,imewataka Watanzania na wawekezaji kutumia fursa ya mikopo ya mabenki katika kuanzisha viwanda hivyo.
“ Nitoe rai kwa taasisi za kifedha za ndani kama TADB, CDRB, NMB na NBC watoe mikopo kwa wawekezaji kuanzisha viwanda vya sukari ili miwa ya wakulima ipate soko” alisema Waziri Mkenda.
Waziri alisema ; “Tunahitaji wawekezaji wengi kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya sukari na sisi kama serikali tutahakikisha Taasisi za fedha ikiwemo Benki ya TADB inatoa mikopo kwa wenye nia ya kujenga viwanda ili kuleta ushindani na hilo ndio litakuwa jawabu la kutatua changamoto ya miwa yao kutopata soko “ alisema Profesa Mkenda.
Waziri wa Kilimo , pia alisema serikali itaendelea kuweka mazingira sawa ili kuwe na ushindani unaouwiana kwa wawekezaji na nchi iwezekuzalisha sukari nyingi kwa kutumia fursa kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kukuza tija na kutumia mbegu bora za miwa.
“Nahimiza uwekezaji katika sekta ya sukari na kuwa serikali itasimamia ushindani ili nchi iwe na uhakika wa uzalishaji na hivyo wawekezaji zaidi wanakaribishwa nchini” alisisitiza Mkenda.
Alisema hatua hiyo ni baada ya kuona viwanda vya sukari vilivyopo havina uwezo mkubwa wa kuchakata miwa yote inayolimwa na wakulima na kwa maana hiyo Serikali imeamua kushawishi wawekezaji wakiwemo wajasiliamali kuwekeza katika viwanda hivyo na itawashika mkono kwa kuhakikisha wanapata mikopo .
Kuhusu suala la sheria na mikataba iliyowekwa miaka ya nyuma kwa ajili ya kuzuia uanzishwaji wa viwanda vya sukari kutoka eneo la umbali wa kilomita 25 kilipojengwa kiwanda kingine ambayo lengo lake lilikuwa nikuvilinda na upatinaji wa malighafi (miwa) kuwa sheria hiyo pamoja na mikataba hazina mantiki kwa nyakati hizi.
Waziri alisema , sheria na mikataba hiyo kwani imeonekana imekuwa ikiwaumiza wakulima wadogo na watu wengine wenye nia ya kuanzisha viwanda vya sukari.
“ Natoa wito kwa wajasilimali wanaohitaji kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata sukari waje tuzungumze na mabenki yawasaidie kutoa mikopo ili kumaliza tatizo hili la upungufu wa sukari” alisema Profesa Mkenda.
Katika hatua nyingine Waziri huyo alikutana na wakulima wa miwa wa Mtibwa ambapo amepokea kero ya miwa yao kununuliwa kwa bei chini ya Sh : 63,000 kwa tani tofauti na ya wakulima wa Kilombero ambao wanauza kwa Sh 120,000 kwa tani.
Akijibu madai ya wakulima hao , Profesa Mkenda alieleza kuwa suluhisho la bei ndogo ya miwa ni kuwa na ushindani mzuri kwa wawekezaji zaidi kuanzisha viwanda vidogo vya sukari hali itakayopunguza utegemezi wa wenye viwanda wakubwa .
Waziri Mkenda pia alitembelea kiwanda cha sukari Mtibwa na kuzungumzia na uongozi wa kiwanda ambapo amewataka kuhakikisha wananunua miwa ya wakulima ili wazalishe sukari zaidi ya tani 50,000 za sasa kwa kuwa kiwanda kina uwezo wa kuzalisha tani 100,000 kwa mwaka.
Hata hivyo ,Waziri Mkenda alirejea agizo lake la kutaka kuona mikataba ya viwanda vya sukari ili ajue kuna nini na wanapaswa kufanya kitu gani zaidi kulingana na mkataba wa ubinafshaji uliofanywa na Serikali mwaka 1999.
“Ni kweli mazingira ya uwekezaji zamani yalikuwa mabaya kwenye uwekezaji wa viwanda vya sukari lakini sasa serikali ya Awamu ya Tano imeboresha sana hivyo tunataka uzalishaji iongezeke” alisema Waziri Mkenda.
Pamoja na hayo ,alisema malalamiko ya wakulima kuhusu bei ya miwa ipatiwe ufumbuzi haraka ili mkakati wa kiwanda wa kuongeza uzalishaji uwe na tija .
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo, (TADB), Japhet Justine alisema katika kuunga mkono jitihada za Rais wamewekeza katika ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Bagamoyo .
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, alisema kwa kipindi cha miezi 24 iliyopita Benki hiyo imetoa kutoa fedha zaidi ya Sh : bilioni 300 katika sekta ya kilimo kwa ujumla.
“Kwa ushirikiano na CRBD na Standard Chartered Benki yetu TADB tumewekeza kwenye uzalishaji wa sukari Bagamoyo ili kuhakikisha nchi inaondokana na uagizaji sukari nje” alisema Japhet.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Albinus Mgonya alisema sekta ya kilimo imechangia mapato ya halmashauri kwa asilimia kati ya 25.9 hadi 34 ambapo katika mwaka 2019/20 iliwezesha halmashauri kutoa mikopo ya shilingi milioni 23 kwa vikundi 30 vinavyojishughulisha na kilimo.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Jonas Van Zeeland , alisema ili kuleta ushindani ni vyema serikali ikaruhusu ujenzi wa viwanda vingine vidogo kwenye eneo la viwanda vikubwa ili wakulima wachaguwe eneo la kupeleka miwa yao hatua ambayo italeta ushindani na suruhisho la matatizo ya wakulima.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo,Mifugo na Maji,Dk Christine Ishengoma , alisema endapo changamoto za wakulima wa miwa hazitapatiwa ufumbuzi itawarudisha nyuma na hiyo kuwa na uwezekano wa kuacha kilimo cha miwa na hamia kwenye mazao mengine ikiwemo mpunga na baadaye kuifanya azma ya serikali kujitosheleza kwa sukari kutofanikiwa.
Mmoja wa wakulima wa miwa ,Seif Hassani , kutoka kijiji cha Mapambano wilayani humo,alisema licha ya kuzalisha miwa lakini mifugo imekuwa ikiwapa hasara kwa kuleta uharibifu wa miwa ikiwa shambani na kuwasababishia kupata hasara kwa kuwa kilimo wanachofanya kinatengemea fedha za mikopo.
Waziri wa Kilimo , Profesa Adolf Mkenda