Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), wakati akizungumza na wananchi wa Kitongoji wa Mwamatome, wilayani Chato, Mkoa wa Geita.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akiwasha umeme katika moja ya nyumba zilizounganishiwa umeme kwenye Kitongoji cha Mwamatome, Kata ya Bwongera, wilayani Chato, Mkoa wa Geita.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akiwasha umeme katika moja ya nyumba zilizounganishiwa umeme kwenye Kitongoji cha Mwamatome, Kata ya Bwongera, wilayani Chato, Mkoa wa Geita.
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani, akiwasha umeme katika moja ya nyumba zilizounganishiwa umeme kwenye Kitongoji cha Mwamatome, Kata ya Bwongera, wilayani Chato, Mkoa wa Geita.
Na Teresia Mhagama, Chato
WAZIRI wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ametoa angalizo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa wamebakiwa na mwezi mmoja na nusu tu wa kuwaunganishia umeme wateja wote waliolipia umeme nchini.
Dkt.Kalemani ametoa angalizo hilo tarehe 17 Februari, 2021, wilayani Chato, Mkoa wa Geita wakati alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya umeme pamoja na kuwasha umeme katika Kitongoji cha Mwamatome na Mkombozi wilayani humo.
“Nilitoa muda wa miezi mitatu wa kuwaunganishia umeme wateja wote waliolipia nchi nzima, mwezi mmoja na nusu tayari mmeshautumia, sasa mmebakiwa na mwezi mmoja na nusu tu, hivyo waunganishieni umeme wateja wote waliolipia.” Amesema Dkt.Kalemani
Kuhusu wateja ambao wanasubiri kupimiwa maeneo yao ili kuunganishwa umeme, amesema kuwa, alishatoa agizo kwa wapimaji wa maeneo wa TANESCO, (surveyors) kununuliwa pikipiki ili kukamilisha upimaji wa maeneo na kwamba ifikapo mwisho wa mwezi wa Pili wawe wameshanunuliwa pikipiki hizo.
Vilevile, kuhusu maendeleo ya kazi ya uunganishaji umeme vijijini nchini, amesema kuwa, hadi sasa jumla ya vijiji 10,263 vimeshaunganishiwa umeme na vijiji vilivyobaki ambavyo vinaendelea kuunganishiwa umeme ni 2,005.
Akizungumza na wananchi wa vitongoji hivyo, Dkt.Medard Kalemani amesisitiza kuhusu matumizi ya kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) ambacho kinawawezesha wananchi kupata umeme bila kuingia gharama za kufunga mfumo wa nyaya katika nyumba.
Pia, amesisitiza kuwa, bei ya kuunganisha umeme vijijini ni shilingi 27,000 tu na kwamba kila nyumba inastahili kupata umeme.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chato, Charles Kabeho, amesema kuwa, kuunganishwa kwa umeme kwenye vitongoji vya Mwamatome na Mkombozi, wilayani humo kutawawezesha wananchi kuweza kufanya biashara mbalimbali na kuanzisha viwanda vidogovidogo.