WAZIRI AWESO ASITISHA AGIZO LA EWURA KUPANDISHA ANKARA ZA MAJI

 

Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso  akizungumza na Watendaji wa Wizara na Taasisi zake katika kikao kazi kilichofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa jijini Dodoma.

………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

Waziri wa Maji Mhe.Juma Aweso amesitisha zoezi lililokuwa likiendelea kwa agizo la Mamlaka  ya Udhibiti wa  Maji na Nishati(EWURA) la kuzitaka mamlaka za maji nchini kupandisha ankara za maji  mpaka hapo atakapojiridhisha na  kuruhusu utaratibu huo kuendelea.

Waziri Aweso ametoa maagizo hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao  kazi cha siku mbili cha wizara ya maji na Taasisi zake ambapo amesema bado hajaridhika na kazi zinazofanywa na mamlaka  hiyo katika eneo la udhibiti katika utoaji wa huduma za maji huku akiwataka kujipanga zaidi. 

Mhe Aweso amesema kuwa EWURA haifanyi vizuri katika udhibiti wa maji wananchi wanabambikiziwa bili bila sababu ya msingi na wao kama wadhibiti wametulia tu.
“Jumatatu nakuja huko nitawakalia kooni kwasababu malalamiko yamekuwa mengi na ninyi kama mamlaka inayohusika na hayo malalamiko mmetulia, nataka nikija mnieleze kwani ni wananchi wanabambikiziwa bili mnawasababishia wananchi wanaona kama wizara haifanyi kazi” amesema Aweso
Aweso aliwataka wakurugenzi wa mamlaka za maji mkoa na wilaya kuhakikisha wanasimamia miradi ya maji ili kuhakikisha maji yanakuwa ya uhakika kwenye maeneo yao kwani hakuna mbadala wa maji.
Aweso pia amewataka wadhibiti ubora wa maji kuhakikisha maji yanayopatikana yanakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu lengo ni kuona wananchi wanaridhika na huduma inayotolewa na sekta hiyo.
“Wakurugenzi msikae ofisi hakikisheni mnatembea miradi ya kuzalisha maji katika maeneo yenu angalau kwa wiki Mara tatu hiyo itasaidia kugundua matatizo ya miradi mapema kabla haijafikia kwenye hatua ya kuleta itilafu wananchi wakakosa maji” amesisitiza

Awali Naibu Waziri wa Maji Mhe. Maryprisca Mahundi, amesema kuwa miradi mingi inayofanya kazi nchini imepitwa na wakati hivyo kuna haja ya kufanya taratibu na Mipango ya kuiboresha kutokana na uchakavu wa miundombinu na vifaa.

Mhe.Mahundi amewataka wataalam kufanya mapitio upya katika miradi hiyo nchi nzima na kuwasilisha taarifa ya namna ya kuikarabati na bajeti nzima itakayohusika kwa ajili ya maboresho.

Amesema kumekuwa na changamoto kubwa katika utekelezaji wa miradi ambayo imekamilika kutokana na jumuiya nyingi za maji kutofanya vizuri katika usimamizi mara baada ya kukabidhiwa miradi hiyo.

 Amesema pia kumekuwa na changamoto ya miradi mingi kutokamilika ili hali akaunti za mameneja zina fedha, jambo hili linasababishwa na mameneja kutojiamini au kukosa kibali cha kutekelezeka majukumu yao kutoka kwa viongozi wa juu.

Kwa upande wake Naibu katibu mkuu wa wizara Maji, Nadhifa Kemikimba amesema hivi sasa kuna changamoto kubwa katika usimamizi wa vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji na uchimbaji madini na shughuli nyingine zinazofanywa na binadamu.

Post a Comment

Previous Post Next Post