WALIMU WAHAMASISHWA KUJIENDELEZA KIELIMU

 

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama (katikati), akifafanua masuala mbalimbali kuhusu wajibu na haki za Walimu, katika mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), Dodoma, Januari 7, 2021.

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama (Meza Kuu), akifafanua masuala mbalimbali kuhusu wajibu na haki za Walimu, katika mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, Dodoma, Januari 7, 2021.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mecktildis Kapinga, akizungumzia kuhusu upandaji madaraja kwa walimu, wakati wa mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), uliofanyika jijini Dodoma, Januari 7, 2021.

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama (kulia) akifafanua jambo kwa Mwalimu Raymond Lyoba kutoka Urambo, Tabora, muda mfupi baada ya kuwasilisha mada kuhusu haki na wajibu kwa walimu katika mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), Januari 7, 2021 jijini Dodoma.

Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mecktildis Kapinga (katikati), akifafanua jambo kwa Mwalimu Huruma Muya kutoka Kigamboni Dar es Salaam (kushoto) na Mwalimu Simon Mwemutsi kutoka Ifakara Morogoro (kulia), muda mfupi baada ya kuwasilisha mada kuhusu haki na wajibu kwa walimu katika mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (hawapo pichani), Januari 7, 2021 jijini Dodoma.

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama (wa tatu-kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu wa Tume, Mecktildis Kapinga (wa tatu-kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, muda mfupi baada ya kuwasilisha mada kuhusu haki na wajibu kwa walimu, Januari 7, 2021 jijini Dodoma.

Sehemu ya wajumbe wa mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, wakifuatilia mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma, Januari 7, 2021.

*********************************************

Na Veronica Simba

Serikali imewahamasisha Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari nchini, kujiendeleza kielimu katika ngazi mbalimbali ili kuboresha zaidi utendaji wao wa kazi.

Wito huo umetolewa jijini Dodoma leo, Januari 7, 2021 na Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama wakati akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara.

Akifafanua, amesema kuwa, kujiendeleza kielimu ni haki ya msingi kwa watumishi wote wa umma wakiwemo walimu, ndiyo maana Serikali kupitia Tume imekuwa ikiwahamasisha kuitumia fursa hiyo ipasavyo.

Chitama amekemea tabia ya baadhi ya Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania Bara, ambao hukataa kutoa ruhusa kwa watumishi walio chini yao wenye nia ya kujiendeleza kielimu.

Hata hivyo, Kaimu Katibu huyo amesisitiza kuwa Walimu wote wa shule za umma wenye nia ya kujiendeleza kielimu, wanapaswa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Mamlaka ikiwemo kufuata Mpango wa Mafunzo.

Aidha, amewasisitiza kuhakikisha wanapata ruhusa ya maandishi kutoka kwa Wakuu wao, kabla ya kwenda masomoni kwani kinyume chake watakabiliwa na mashtaka ya utoro kazini ambayo adhabu yake ni kufukuzwa kazi.

 “Tumekuwa tukipata rufaa nyingi za kesi za Walimu ambao walitoroka kazini na kwenda masomoni hivyo kufukuzwa kazi. Serikali inapenda walimu msome lakini fuateni taratibu zilizowekwa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka TSC, Mecktildis Kapinga, akifafanua kuhusu utaratibu wa kupanda vyeo, ameueleza Mkutano huo kuwa, kanuni inaelekeza kutompandisha cheo mtumishi yeyote wa umma akiwa masomoni, hadi pale anapohitimu ndipo mchakato wa kumpandisha hufanyiwa kazi.

“Naomba mtambue kuwa utaratibu huo ni kwa watumishi wote wa umma, na siyo kwa walimu pekee kama ambavyo baadhi yenu mmekuwa mkinung’unika,” amefafanua Kapinga.

Mkutano huo wa siku tatu, ulianza Januari 5, 2021 huku ukiongozwa na kaulimbiu isemayo uongozi na usimamizi makini wa elimu, utaimarisha Tanzania katika uchumi wa kati.

Tume ya Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa walimu wa shule za msingi na sekondari Tanzania Bara, walio kwenye utumishi wa umma

Post a Comment

Previous Post Next Post